NYOTA WA WIKI: Pierre-Emerick Aubameyang

NYOTA WA WIKI: Pierre-Emerick Aubameyang

Na GEOFFREY ANENE

PIERRE-Emerick Aubameyang ni mmoja wa nyota kambini mwa FC Barcelona.

Auba, ambavyo anafahamika kwa jina la utani, alijiunga na miamba hao wa Uhispania kutoka Arsenal, Uingereza mwezi Januari 2022.

Katika mechi nne amechezea Barca, mshambulizi hodari kutoka Gabon tayari ameonyesha ni katili langoni.

Mnamo Februari 20, mchezaji huyo bora wa Afrika 2015 alidhihirisha bado yuko fiti alipomaliza ukame wa mechi 15 bila bao (michuano mitatu kwenye La Liga) kwa kutetemesha nyavu za wenyeji Valencia mara tatu Barcelona ikiibuka na ushindi wa 4-1.

Ametoka mbali kufika kuwa mmoja wa wachezaji stadi wa soka. Aubameyang hakulelewa Gabon wala Ufaransa alikozaliwa bali Milan nchini Italia. Babake Pierre Aubameyang alikuwa skauti wa klabu ya AC Milan. Babake aliyekuwa beki matata enzi zake, alichangia pakubwa katika kunoa talanta ya wanawe watatu.

Auba,32, ana ndugu zake wakubwa William-Fils,35, na Catilina,38, pia waliokuwa wanasoka. Alianza kuonyesha uweledi wake akiwa Saint-Etienne alipoifungia mabao 41 na kusuka pasi 25 katika mechi 97 alizoisakatia kati ya Januari 31, 2011 na Mei 2013.

Aliendelea kuwa mwiba mkali kwa wapinzani alipojiunga na Borussia Dortmund mnamo Julai 2013. Alihama Dortmund akiwa ameifungia mabao 141 na kumega pasi 36 zilizozalisha magoli katika jumla ya michuano 213.

Anafahamika kwa kasi ya kutisha na makombora makali. Ni mzuri katika kukamilisha mashambulizi na pia kumiliki mpira.

Auba, ambaye aliwahi kuhusishwa na klabu nyingine kubwa zikiwemo Manchester City na Real Madrid, pia ni mbunifu. Aliondoka ugani Emirates akiwa ameifungia magoli 92 katika mechi 163 tangu ajiunge na Arsenal mnamo Januari 2018.

Kwa muda mrefu, Auba alikuwa winga kabla ya kocha Jurgen Klopp kumbadilisha kuwa mshambulizi wa kati wakati Robert Lewandowski aliondoka Dortmund na kujiunga na Bayern Munich mnamo Julai 2014.

Mchezaji huyo anayefahamika kwa kufingirika anaposherehekea kufunga bao, ana mke Alysha Behague na watoto wawili.

Akiwa na mabao 30, Auba ndiye mfungaji bora wa Gabon. Aliwahi kuitwa katika timu ya taifa ya Italia ya Under-19 na pia kuchezea Ufaransa under-21 miaka yake ya mwanzo ya uchezaji.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ni unyama wanataaluma kutumia ujuzi wao...

Messi, Ronaldo au Morata kusimamia harusi Dybala, Gabriela

T L