NYOTA WA WIKI: Victor Osimhen

NYOTA WA WIKI: Victor Osimhen

NA GEOFFREY ANENE

VICTOR Osimhen anaongoza ufungaji wa mabao kwenye mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) 2023 nchini Ivory Coast.

Mshambulizi huyo, ambaye bei yake inaaminika kufika Sh12.3 bilioni, alitinga bao moja Nigeria ikianza kampeni ya Kundi A kwa kulemea Sierra Leone 2-1 Juni 9 mjini Abuja kabla ya kuongeza magoli manne Super Eagles ikilipua wanavisiwa wa Sao Tome & Principe 10-0 Juni 13 mjini Agadir, Morocco.

Vic anavyofahamika Osimhen kwa jina la utani, alianza uanasoka katika akademia ya Ultimate Strikers jijini Lagos familia yake ilipohamia huko kutoka jimbo la Edo.

Uchezaji wa kuvutia ulifanya mshambulizi wa zamani wa Zamalek na Barcelona na Nigeria, Emmanuel Amunike amjumuishe katika timu ya taifa ya Nigeria Under-17 mwaka 2015.

Hiyo ilimpa fursa ya kujinadi zaidi kwa maskauti kutoka Bara Ulaya kwenye Kombe la Dunia 2015 nchini Chile.

Aliridhisha kwa kuibuka mfungaji bora kwa mabao 10 na kumezewa mate na Arsenal, Manchester City na Tottenham Hotspur kutoka Uingereza.

Hata hivyo, Victor, ambaye alituzwa chipukizi bora wa mwaka Afrika 2015 akiwa bado Ultimate Strikers na pia kubeba taji la Kombe la Afrika Under-23 mwaka huo, alipuuza klabu hizo na kujiunga na Wolfsburg mapema 2017.

Mambo yalikuwa magumu Wolfsburg, hasa kutokana na kusumbuliwa na majeraha na pia kukosa kujiamini.

Wolfsburg ilimsukuma Charleroi msimu 2018-2019 kabla ya kuuzia klabu hiyo ya Ubelgiji mwanasoka huyo Julai 2019 kwa ada ya Sh435 milioni. Kisha, aliingia Lille nchini Ufaransa mnamo Agosti 1, 2019 kwa Sh2.7 bilioni baada ya kufuma wavuni mabao 20 katika michuano 36.

Hakuchelewa kuendelea kutesa makipa kwenye Ligue 1 msimu 2019-2020 akifungia Lille mabao 18 katika mechi 38 za mashindano yote na kusuka pasi sita zilizozalisha magoli sita. Alitawazwa mchezaji bora kambini Lille msimu huo kabla ya kunyakuliwa na Napoli kwa ada inayoaminika kuwa kati ya Sh9.3 bilioni na Sh10.5 bilioni.

Vic anajivunia mabao 28 na pasi tisa zilizoishia kutiwa nyavuni kambini Napoli.

  • Tags

You can share this post!

Ruto, Raila walenga kudhibiti mabunge

Mimi niende Newcastle? Acheni hizo!

T L