Michezo

Nyota walioshindia AFC Leopards taji mwaka 1998 na shughuli wanazofanya miaka 22 baadaye

May 24th, 2020 3 min read

Fahamu nyota walioshindia AFC Leopards taji la mwisho la Ligi Kuu miaka 22 iliyopita

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya AFC Leopards ilishinda Ligi Kuu ya mpira wa miguu ya Kenya mwaka 1998.

Tangu wakati huo, imekuwa ikitamani kuimarisha idadi ya mataji yake 13 bila mafanikio. Ni miaka 22 sasa tangu ipate ufanisi huo chini ya kocha Sunday Kayuni kutoka Tanzania, ambaye alikuwa amechukua usukani katikati ya msimu kutoka kwa Flemming Jacobsen.

Mwaka 1998, Leopards almaarufu Ingwe ilikuwa na mwenyekiti Francis Chahonyo, ambaye sasa ni marehemu. Naibu kocha wa timu hiyo alikuwa Martin Ndagano kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo nao Alfred Imonje na Gilbert Selebwa walihudumu kama meneja wa timu na naibu meneja wa timu, mtawalia.

Ukumbi huu unaangazia kikosi cha wachezaji kilichoshindia Ingwe taji hilo la mwisho.

Matthew Owino Ottamax na Mohammed Fwaya waling’ara michumani katika kunyakia Ingwe mipira. Walibadilishana michumani msimu huo. Ottamax sasa ni balozi wa spoti katika kilabu cha 40Forty Lounge kinachopatikana katika mtaa wa Runda na pia Westlands.

Ottamax anaishi katika mtaa wa Lavington. Baada ya kuangika glavu zake, alijaribu bahati katika ukocha jijini Nairobi katika akademia ya Ujuzi Soccer Academy na pia shule ya Aga Khan Junior & Senior kabla ya kuwa kocha wa makipa katika klabu za Nairobi City Stars, Gor Mahia, Nakumatt na Leopards wakati tofauti na pia timu ya taifa ya Harambee Stars.

“Kwa wakati huu nipo kwenye ulingo wa burudani pale 40Forty Lounge kama balozi wa kilabu hiki wa masuala ya spoti. Napatia wanamichezo ari kuwa kuna maisha baada ya kustaafu michezoni,” Ottamax aliambia Taifa Leo katika mahojiano.

Mwandishi huyu hakuweza kupata habari kuhusu Fwaya, ingawa kipa huyu aliwahi kuwa kocha wa makipa katika klabu ya Leopards. Katika enzi zake kama mchezaji, Fwaya alicheza soka ya malipo nchini Qatar na pia kuwa kipa wa Harambee Stars.

Francis Baraza ni kocha mkuu wa Biashara Mara United nchini Tanzania. Baada ya kustaafu uchezaji, Baraza amezunguka klabu nyingi nchini akizinoa. Aliwahi kuongoza SoNy Sugar na Western Stima na kuwa naibu wa kocha Tusker kabla ya kuyoyomea Chemelil Sugar na kisha kuvuka mpaka hadi nchini Tanzania kufundisha Biashara inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Somo wake Francis Oduor pia alikuwa beki matata wa Ingwe akiingoza kutwaa taji la mwisho 1998 akiwa nahodha. Oduor ametumikia klabu kadhaa kama kocha.

Alikuwa Wazito kabla iingie Ligi Kuu kwa mara ya kwanza mwaka 2017 na pia alisaidia Kisumu All Stars kupandishwa daraja kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kabisa msimu huu wa 2019-2020.

Alifanywa kuwa naibu wa kocha All Stars ilipoingia Ligi Kuu, huku kocha mkuu akiwa Henry Omino, ambaye majuma machache yaliyopita aliaga dunia.

“Kwa sasa, mimi siko Kisumu All Stars. Niko hapa Luanda, Kaunti ya Vihiga nakitoa huduma zangu kwa klabu ya Luanda Villa,” Oduor alisema.

Majagina Nicholas Muyoti, Simeon Mulama, Chris Ojiambo, Eric Bwabi, Marius Mugisha na George Sunguti pia walikuwa katika kikosi cha Ingwe kilichoibuka mfalme wa mwaka 1998.

Muyoti sasa ni kocha mkuu wa Kakamega Homeboyz inayofanya vyema kwenye Ligi Kuu. Aliwahi kuwa naibu kocha na pia kocha mkuu wa Leopards na Thika United na kocha mkuu wa Oserian na Nzoia Sugar kabla ya kutua Homeboyz.

Mulama, ambaye aliwahi kusakata soka yake nchini Misri, Amerika na Uswidi kabla ya kumalizia alikoanzia Mathare United, ni mkurugenzi wa soka katika klabu ya Gogo Boys inayoshiriki ligi ya daraja ya nne nchini Kenya. Aliajiriwa na Gogo Boys mwezi Februari 2020 kwa sharti la kuhakikisha inaingia Ligi Kuu mwaka 2023.

Ojiambo yuko nchini Amerika, sawa na Richard Asabe na Austin Makacha. Bwabi, Mugisha na John Magwe ni marehemu.

Sunguti, ambaye alitandaza soka yake pia katika mataifa mengi (Uganda, Uswidi, Vietnam na Tanzania), amekuwa kocha wa timu ya Kaunti ya Nairobi katika michezo baina ya kaunti za Kenya (KICOSCA).

Hata hivyo, anafahamika zaidi kama meneja wa uwanja wa City Stadium jijini Nairobi.

Nao Wycliffe Jumba, Evans Majani na Paul Ochieng’ wanafanya shughuli mbalimbali jijini Nairobi. Ramadhan Balala anafanya kazi na wanaumeme wa Western Stima mjini Kakamega.

Philip Ouma yuko nchini Uganda naye Bushuru ni mkazi wa Kitale. Washambuliaji Boniface Ambani na Fred Ambani wapo jijini Nairobi.

Boniface, ambaye ni mdogo wa Fred, amezamia biashara ya michezo baada ya kuwa kocha wa machipukizi Leopards. Fred ni kocha wa klabu ya Wazito.