Michezo

Nyota wapasha miguu moto tayari kuihama Arsenal

June 3rd, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MUINGEREZA Emile Smith Rowe huenda akapata makao mapya Fulham ama Napoli baada ya ripoti kuwa klabu hizo zinatamani kumsaini soko litakapofunguliwa Juni 14 hadi Septemba 2.

Kiungo huyo mshambulizi amewahi kumezewa mate na Aston Villa, Chelsea na West Ham, lakini sasa kuna uwezekano mkubwa atahama klabu yake ya Arsenal baada ya kuwa na mchango mdogo sana msimu 2023-2024.

Katika msimu huo, Smith Rowe alisakata michuano 19 (13 kwenye Ligi Kuu, tatu katika Klabu Bingwa Ulaya na moja kila moja katika Kombe la FA na Kombe la Carabao). Hakupata bao katika mechi hizo, akifanikiwa asisti mbili ligini.

Smith Rowe, 23, ambaye aliwahi kuzichezea Leipzig nchini Ujerumani na Huddersfield Town kwa mkopo, amekuwa kambini mwa Arsenal tangu mwaka 2010 akitokea Glebe FC.

Licha ya kuwa Arsenal waliweka bei yake sokoni kuwa  Sh10.1 bilioni (Pauni 60 milioni) kabla ya mwaka 2024 kuanza, mchango mchache wa Smith Rowe ugani Emirates umeshuhudia thamani yake ikishuka kutoka Sh5.7 bilioni (Yuro 40 milioni) mwezi Machi 2022 hadi Sh3.1 bilioni (Yuro 22 milioni) mnamo Mei 27, 2024.