MakalaSiasa

JAMVI: Nyota ya Jumwa itang'aa licha ya kutimuliwa ODM?

March 10th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

Nyota ya mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa, huenda ikang’aa iwapo atavuka vizingiti vyote baada ya kutimuliwa na chama cha ODM na hata kukamilisha kipindi chake bungeni kwa tiketi ya chama hicho.

Mbunge huyo amepuuzilia mbali kufurushwa kwake ODM na kusema kwamba ataendelea kuhudumu hadi 2022. Tayari amepata agizo la kuzuia chama hicho kumtimua huku wadadisi wakisema kuna uwezekano kwamba atakuwa mbunge hadi kipindi chake cha kuhudumu kitakapokamilika.

“Bi Jumwa anaweza kuwa alifukuzwa ODM lakini ana haki ya kukata rufaa katika jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa na amefanya hivyo. Hata kama jopo hilo litaidhinisha uamuzi wa ODM wa kumtimua, ana haki ya kwenda mahakamani kutatufa haki. Ninachojua, na kile ODM inachojua ni kwamba itachukua muda kwake kukamilisha mfumo wote na ODM italazimika kusubiri,” alisema mbunge mmoja ambaye hakutaka tutaje jina lake kwa sababu ya uhusiano wake na viongozi wa chama cha ODM.

Bi Jumwa aliwaambia wakazi wa eneobunge lake kwamba hakuna uchaguzi mdogo utakaofanyika baadhi ya watu wanavyodai.

“Sihitaji kuomba mtu yeyote msamaha kutokana na uamuzi wangu, kura ni za Malindi na sisi ndio Wanamalindi na ningependa kuwaambia kuwa hakutakuwa na uchaguzi wowote hapa, wafanyabiashara waendelee na shughuli zao bila woga,” alisema siku moja baada ya ODM kuamua kumtimua.

Wadadisi wanasema ujasiri wake unatokana na uungwaji mkono mashinani na jinsi chama hicho kilivyofikia uamuzi wa kumfukuza na kumsamehe mbunge wa Msambweni Suleiman Dori licha kusema awali kwamba uamuzi wa kuwafukuza ulikuwa wa mwisho.

“Katika mazingira ya sasa ya siasa, chama hakiwezi kuamua kufukuza mbunge aliyechaguliwa kisha apoteze kiti chake mara moja. Ni lazima utaratibu wote wa kisheria ufuatwe. Mbunge huwa anachaguliwa na watu na hata kwa wapigakura, ni mlima kumfuta kazi,” asema mdadisi wa siasa Benard Omwaka.

Anatoa mfano wa chama cha Narc Kenya kilipomfukuza Mike Sonko alipokuwa mbunge wa Makadara kwa kumuunga mgombeaji wa chama tofauti kwenye uchaguzi wa eneobunge la Kamukunji.

Bw Sonko alienda mahakamani na kupata agizo la kuzuia msajili wa vyama vya kisiasa kufuta jina lake kama mwanachama wa chama hicho. “Sonko alihudumu hadi mwisho wa kipindi chake na umaarufu wake ukaongezeka hadi leo ni Gavana wa Nairobi. Sio ajabu hatua ya ODM ikafanya nyota ya Bi Jumwa kung’aa zaidi badala ya kuzimika,” alisema Bw Omwaka.

Wadadisi wanasema masaibu ya Bi Jumwa yanatokana na mazingira sawa na yaliyomwandama Bw Sonko wakati huo. ODM kinamshtumu kwa kukiuka kanuni za chama na kudharau viongozi baada ya kutangaza kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto.

Bi Jumwa anadai kwamba hakupatiwa nafasi ya kujitetea na kwamba chama hicho hakikufuata sheria. Kulingana na wadadisi, uamuzi wa chama wa kumsamehe Bw Dori unaweza kuwa baraka kwa Bi Jumwa hata kama uchaguzi mdogo utafanyika na agombee kwa kiti tofauti.

“Taswira iliyojitokeza na ambayo inaweza kufanya nyota ya mbunge huyo kung’aa kwenye uchaguzi mdogo iwapo utafanyika ni ile ya kubaguliwa. Wapigakura wa Malindi watajiuliza kwa nini ni Jumwa pekee aliadhibiwa na kuna wanasiasa wengi wa ODM ambao wamekuwa wakiandamana na Bw Ruto,” asema Bw Omwaka.

Tayari wakazi wa Malindi wamelaumu ODM kwa kumdhulumu mbunge wao. Kulingana na mwenyekiti wa chama hicho eneobunge la Malindi Hossea Chome, chama kilipuuza haki za Bi Jumwa.

Hii inaonyesha kwamba anaungwa mkono mashinani japo kuna wanaosubiri kupambana naye iwapo uchaguzi mdogo utafanyika. Wadadisi wanasema ni ujasiri wa mbunge huyo na weledi wake wa kucheza siasa ambao utamkweza kisiasa.

“Kumbuka wakati wa kampeni cha uchaguzi alivyokuwa jasiri kupigia debe chama cha chungwa sio tu eneo la pwani mbali kote nchini. Japo siasa ni telezi sidhani ni rahisi kummaliza Bi Jumwa kisiasa kwa kumfukuza chamani,” alisema mdadisi wa siasa Abdullahi Hassan.

Bw Hassan anasema kufikia sasa ODM kimeonyesha kumfukuza Bi Jumwa kulichangiwa na mambo tofauti na yale kilichodai kiliposema hakitabatilisha uamuzi wa kumtimua Bi Jumwa.

“Ninadhani hakikuwa na sababu ya kumtimua chamani isipokuwa visingizio kwa sababu kinajua lazima angekata rufaa kwa jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa na hata mahakamani,”

“Kusema haitabatilisha uamuzi wake ni sawa na kusema hakitaheshimu mahakama ikikubaliana na Bi Jumwa. Kufanya hivyo kutamfanya mbunge kuwa shujaa,” asema Bw Hassan.

Mwenyekiti wa chama hicho John Mbadi alinukuliwa akisema kimefunga ukurasa wa Bi Jumwa na akawakashifu wanaokosoa uamuzi wa kumtimua. Bw Hassan anasema ODM kinafaa kubaini uamuzi wake hautaweza kuzima nyota ya Bi Jumwa kufuatia idadi ya wabunge wa pwani wanaomuunga mkono.

Wabunge wengine wa pwani kama vile Owen Baya (Kilifi Kaskazini), Michael Kingi (Magarini),Gertrude Mbeyu (mwakilishi wa wanawake) na mbunge wa Kaloleni Paul Katana. Wabunge hao pia wamekuwa wakiandamana na naibu wa Rais William Ruto katika mikutano ya hadhara na michango wakiahidi kufanya kazi naye na hawajachukuliwa hatua.