MakalaSiasa

Nyota ya kisiasa ya Isaac Ruto yaanza kung’aa tena

December 18th, 2018 2 min read

TOM MATOKE na WYCLIFF KIPSANG

ALIYEKUWA Gavana wa kwanza wa Bomet, Bw Isaac Ruto, anazidi kuonekana kupata mwamko mpya kisiasa katika Bonde la Ufa mwaka mmoja baada ya kushindwa uchaguzini na Dkt Joyce Laboso.

Wiki chache baada ya Naibu Rais William Ruto kutangaza kuwa wametatua tofauti zilizokuwepo kati yake na kiongozi huyo wa Chama Cha Mashinani, wanasiasa wa eneo hilo sasa wamejitokeza kumpa majukumu mapya.

Viongozi kutoka Kaunti ya Nandi walisema gavana huyo wa zamani atahitajika kumpatanisha naibu rais na wabunge waasi wa Chama cha Jubilee Rift Valley.

Wabunge ambao wamekuwa wakimshambulia vikali naibu rais eneo hilo na kutishia kuyumbisha azimio lake la kuwa rais 2022 wanaongozwa na Alfred Keter (Nandi Hills), Joshua Kutuny (Cherangany) na Silas Tiren (Moiben).

Gavana wa Nandi, Bw Stephen Sang, Seneta Samson Cherargei, Mbunge wa Mosop Vincent Tuwei na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kaunti ya Nandi, Bw Charles Tanui, walisema naibu rais hatafanikiwa kushinda urais ikiwa jamii ya Wakalenjin imegawanyika.

Walimtaka aliyekuwa gavana wa Bomet kushauriana na wabunge hao waasi ili jamii iwe na msimamo mmoja wa kisiasa.

“Kama viongozi wa Kaunti ya Nandi, tunamtwika jukumu aliyekuwa Gavana wa Bomet na Bw Tuwei waandae mkutano wa upatanisho na wabunge hao watatu,” akasema Bw Sang.

Walisema ni muhimu watatu hao wamtambue naibu rais kama kigogo wa kisiasa Rift Valley ili afanikiwe kushinda urais kwani mgawanyiko wa jamii utagawanya kura zao kwa wagombeaji mbalimbali wa urais.

“Ushindi hautapatikana ikiwa wabunge hao watatu na wapinzani wengine wa naibu rais hawako pamoja na jamii nzima,” akaongeza gavana huyo.

Seneta Cherargei alionya viongozi dhidi ya kumdharau naibu raia akasema wanaofanya hivyo wanahatarisha nafasi zao za kushinda tena nyadhifa za kisiasa ifikapo 2022.

Kulingana naye, Bw Ruto ndiye alichukua mwenge wa kuongoza jamii ya Wakalenjin kisiasa tangu Rais Mstaafu Daniel arap Moi alipostaafu katika mwaka wa 2002.

Mbali na wabunge hao watatu wa Jubilee, Seneta wa Baringo Gideon Moi pia ameibuka kuwa hasimu mkubwa wa naibu rais katika eneo hilo.

Ingawa seneta huyo hajatangaza wazi kama anaazimia kuwania urais 2022, inaaminika chama anachoongoza cha KANU kitaungana na vyama vingine ambavyo huenda vikawa na mpinzani wa Bw Ruto.

Bw Tuwei alisema: “Viongozi wote waliochaguliwa katika jamii ya Wakalenjin lazima waeke kando tofauti zao za kisiasa na wamuunge mkono naibu rais. Tunataka kusikiliza malalamishi ya wabunge hao watatu kumhusu naibu rais.”

Juhudi za wazee wa jamii hiyo kuwapatanisha wabunge hao na naibu rais hazijafua dafu, na sasa inasubiriwa kuonekana kama wapatanishi walio wanasiasa watafanikiwa kutatua uhasama uliopo.