Makala

Nyota ya Waiguru yaendelea kung’aa tangu ajinasue kwa sakata ya NYS

March 29th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

KWA wengi, ingali fumbo kwamba Gavana Anne Waiguru (Kirinyga) ndiye mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG).

Naam, mwanamke wa kwanza kuwa mwenyekiti wa baraza hilo lenye ushawishi mkubwa katika uendeshaji wa mfumo wa ugatuzi nchini.

Wadadisi wanamtaja Bi Waiguru kama mtu ambaye nyota yake ya kisiasa imeota na kung’aa  katika mazingira tatanishi sana.

Mnamo 2015, Bi Waiguru alilazimika kujiuzulu kama Waziri wa Ugatuzi, baada ya kuhusishwa na tuhuma za uporaji wa zaidi ya Sh791 milioni katika Shirika la Kitaifa la Vijana (NYS).

Licha ya baadhi ya maafisa wa ngazi za juu katika serikali ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kujaribu kumtetea, Bi Waiguru alilazimika kujiuzulu kutokana na shinikizo na lawama nyingi zilizokuwa zikielekezwa kwake.

“Nimeamua kujiuzulu kutokana na ushauri wa daktari wangu, na kutoa nafasi kwa asasi husika kufanya uchunguzi wake,” akasema Bi Waiguru, kwenye kikao cha habari kilichokumbwa na taharuki.

Baada ya joto kutulia, Bi Waiguru aliwashangaza wengi kwa kuamua kuwania ugavana katika Kaunti ya Kirinyaga kwa tiketi ya Chama cha Jubilee (JP), kilichokuwa maarufu sana katika ukanda wa Mlima Kenya.

Bi Waiguru, alitangazwa mshindi dhidi ya aliyekuwa gavana wa kwanza katika kaunti hiyo, Bw Joseph Ndathi.

Baada ya ushindi huo wa kimiujiza, Bi Waiguru alikumbana na kibarua kingine.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2022,  wengi walitabiri kwamba Bi Waiguru angebwagwa na aliyekuwa Mwakilishi wa Kike katika kaunti hiyo, Bi Wangui Ngirichi.

Hili lilitokana na kampeni kali ambazo Bi Ngirici alikuwa amefanya—kwa usaidizi wa mumewe, Bw Andrew Ngirici.

“Bila shaka, wengi waliamini kwamba muhula na wakati wa Bi Waiguru kama gavana wa Kirinyaga ulikuwa umefikia kikomo. Hata hivyo, aliwashangaza wengi baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kumtangaza kama mshindi,” asema Bw Ndung’u Chege, ambaye ni mdadisi wa siasa ma mkazi wa Kirinyaga.

Anasema kuwa hadi leo, wakazi wengi bado hushangazwa na jinsi Bi Waiguru alifanikiwa kuhimili wimbi na umaarufu mkubwa aliokuwa nao Bi Ngrici.

Kwa sasa, ikizingatiwa kuwa Bi Waiguru anahudumu katika muhula wa pili na wa mwisho kama gavana, baadhi ya watu wanasema kuwa kama mwanamke mwanasiasa, yu miongoni mwa viongozi ambao huenda wakashikilia nyadhifa kubwa katika serikali itakayobuniwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2027.

“Bi Waiguru amejidhihirisha kama kiongozi ambaye si wa kudharauliwa. Kwa sasa, anahudumu kama mwenyekiti wa CoG. Hilo pekee limemkweza na kumpandisha hadhi kama kiongozi mwanamke mwenye uwezo mkubwa wa kisiasa. Hali ilivyo, anabaki kuwa miongoni mwa viongozi wanaofaa kutazamwa sana baada ya uchaguzi wa 2027,” asema mdadisi wa siasa Dismus Mokua.