Habari Mseto

NYS: Family Bank yakiri kukiuka sheria

December 18th, 2018 2 min read

Na Richard Munguti

BENKI ya Family (FBL) Jumatatu ilikiri kuwa ilikaidi sheria kwa kumruhusu msusi wa nywele Josephine Kabura kuchukua mamilioni ya pesa katika sakata ya Sh791milioni iliyokumba shirika la huduma ya vijana kwa taifa (NYS).

Wakili Waweru Gatonye alimueleza Hakimu Mkuu, Bw Francis Andayi kuwa FBL imekubali kulipa faini ya Sh64,500,000 kwa kukiuka sheria zinazodhibiti usimamizi wa benki.

“FBL imekubali italipa faini ya Sh64,500,000 kwa kutopiga ripoti kwamba mteja wake alikuwa anatoa zaidi ya Dola za Marekani $10,000 (sawa na Sh1,000,000) bila kupiga ripoti,” kiongozi wa mashtaka Bi Lilian Obuor alimueleza Bw Andayi.

Bi Obuor alisema FBL iko tayari kulipa faini hiyo.

Kulingana na mkataba huo FBL italipa NYS Sh24,500,000 na Sh40milioni zitalipwa mahakama.

Mkataba huo ulitiwa saini Desemba 11, 2018 na wakili wa benki hiyo, Bi Rebecca Mbithi naye naibu wa DPP, Bi Dorcus Oduor ametia saini kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bw Noordin Haji.

“Niko na mkataba wa maelewano kati ya FBL na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kuhusu makubaliano hayo,” alithibitisha Bi Obuor.

Mkataba huo ulithibitishwa na wakili Waweru Gatonye anayewakilisha benki hiyo.

Bw Gatonye aliomba Mahakama ipokee mkataba huo wa maelewano upokewe na kukubaliwa na mahakama.

Lakini mwakilishi wa FBL aliyejibu mashtaka kesi ilipowasilishwa mahakamani Bw John King’ori alimweleza Bw Andayi “hajui chochote kuhusu mkataba uliofikiwa kati ya DPP na FBL.”

“Mimi sijui ikiwa kuna mkataba wa kuondoa mashtaka dhidi ya benki ya FBL,” Bw King’ori ambaye ni afisa mkuu wa masuala ya usalama was benki alimueleza hakimu.

Bw Andayi alighadhabishwa na matamshi hayo na kutisha kumsukuma afisa huyo wa benki ndani.

Baada ya mashauriano , Bw Andayi aliamuru ripoti hiyo ikabidhiwe washtakwa.

Wakuu wa FBL walioshtakiwa pamoja na Bw King’ori ni afisa mkuu FBL Bw Peter Munyiri , Bw Robert Oscar Nyagah, Bw Charles Kamau Thiong’o na Bw Raphael Mutinda Mutinda Mutiso.

Wengine walioshtakiwa ni Bi Nancy Njabi, Meldon Awino Onyango, Josephine Njeri Wairi na FBL.

Bw King’ori aliomba apewe muda wa kusoma mkataba huo wa maelewano ndipo ajue atakachoambia korti.

Kwa mujibu wa mkataba huo mahakama imeelezwa kuwa FBL haijashurutishwa kukiri mashtaka tisa ya kukaidi sheria zinazothibiti benki kwa kutoripoti kuwa Bi Kabura alikuwa anatoa mamilioni ya pesa ambazo kampuni zake zilikuwazimepokea kutoka kwa NYS.

Benki hiyo imekiri kuwa haikupiga ripoti kwa Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwamba ilishuku Bi Kabura alikuwa akishiriki katika ulanguzi wa pesa.

“Mshtakiwa (FBL) amekiri mashtaka ya kukaidi sheria za benki kwa kutoripoti utoaji wa viwango vikubwa vya pesa,” mkataba huo umeeleza.

Washtakiwa wamedaiwa walifanya makosa hayo kati ya Desemba 22, 2014 na Mei 19, 2015 kati tawi la FBL katika jengo la KTDA, Nairobi..

Washtakiwa wamekana walikosa kuripoti kuwa kampuni ya Reinforced Concrete Technologies inayomilikiwa na Bi Kabura ilikuwa inatoa pesa zinazozidi Sh1,000,000.

Pia wameshtakiwa kwa kumruhusu Bi Kabura kujiuhusisha na ulanguzi wa pesa wa zaidi ya Sh 320,160,000.

Washtakiwa wako nje kwa dhamana.