Habari Mseto

NYS: Polisi ashtakiwa kwa kutolipa ushuru kwa KRA

October 25th, 2019 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

AFISA wa polisi aliyelipwa mamilioni ya pesa na Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) baada ya kutoa huduma tofauti alishtakiwa Alhamisi kwa kukwepa kulipa ushuru wa zaidi ya Sh8 milioni huku Phyilis Njeri Ngirita, mmoja wa washukiwa wanaoshtakiwa kuhusiana na kashfa ya Sh791 milioni NYS, akiangua kilio mahakamani kutokana na masaibu anayopitia.

 

Afisa huyo wa polisi Bi Caroline Atieno Mango, alishtakiwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Bernard Ochoi, katika mahakama ya Milimani Nairobi.

Bi Mango alikanusha mashtaka 20 aliyofunguliwa na mamlaka ya ushuru nchini KRA ya kukwepa kutoa ushuru kati aya 2014 na 2019 ilhali alilipwa mamilioni ya pesa na NYS.

“Mshtakiwa huyu anakabiliwa na mashtaka ya kukwepa kulipa zaidi ya Sh8milioni kwa Serikali,” alisema kiongozi wa mashtaka Bi Doris Ing’ahizu.

Bi Ing’ahizu alimsihi hakimu amwachilie mshtakiwa kwa kiwango cha juu cha dhamana mbali na kumwagiza asivuruge uchunguzi unaoendelea dhidi ya watoto wake watatu Peris, Ian na Brianna waliofanya biashara na NYS na kulipwa na pia wakakwepa kulipa kodi.

“Maafisa wa KRA wanaendelea kuwachunguza watoto wake mshtakiwa kwa kukwepa kulipa kodi. Naomba hii mahakama imwamuru Atieno asithubutu kuvuruga uchunguzi na kuhujumu haki,” aliomba Bi Ing’ahuzu.

Lakini Bi Mango aliomba aachiliwe kwa dhamana na kuonywa “asivuruge uchunguzi na kwamba atafika kortini atakapohitajika.

Bi Mango alisema amekuwa nje kwa dhamana ya polisi ya Sh30,000 na “hakuna siku hata moja alikosa kujisalimisha kuhojiwa wakati wa kipindi hicho chote cha uchunguzi.”

Naye Phyilis alimweleza hakimu mkuu Martha Mutuku hawezi kujikimu kimaisha na hata ameshindwa kumlipia mtoto wake karo.

Mtoto wake huyo ambaye baba yake ni raia wa Ujerumani amemtaka ambadilishie jina kwa vile “amekuwa akichekwa shuleni kwamba mama yake ni milionea ilhali hawezi kumlipia karo.”