Habari Mseto

NYS sasa kutegemea mapato yake kujiimarisha

January 2nd, 2019 2 min read

Na CHARLES WASONGA

MSWADA unaolenga kuimaisha usimamizi wa Shirika la Vijana kwa Huduma kwa Taifa (NYS) na kuipa sura mpya baada ya kuzongwa na ufisadi tangu 2015 umetiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta.

Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi na mwenzake wa Seneti Ken Lusaka waliwasilisha mswada huo kwa Rais katika Ikulu ya Mombasa ambapo aliwaongoza Wakenya kualika Mwaka Mpya wa 2019.

Mswada huo maarufu kama “National Youth Service (NYS) Bill” unaibadili sura ya shirika hilo kuwa Shirika la Kiserikali ambalo majukumu yake yatahusisha uendeshaji wa shughuli za uzalishaji mali, utengenezaji bidhaa na shughuli nyinginezo za mapato.

Muhimu ni kwamba, tofauti na hali ilivyokuwa zamani, chini ya sheria hii mpya NYS itakuwa ikizalisha mapato yake badala ya kutegemea, kwa kiwango kikubwa, mgao wa fedha kutoka Serikali ya Kitaifa.

Waziri wa Utumishi wa Umma, Vijana na Masuala ya Jinsia Profesa Margaret Kobia alisema chini ya sheria hiyo baraza la watu 12 ambao watasimamia utendakazi wa NYS.

“Vile vile, chini ya sheria hii, mkaguzi wa hesabu atateuliwa kufuatilia matumizi ya fedha katika NYS”, akasema Waziri Kobia ambaye pia alishuhudia kutiwa saini kwa mswada huo.

“Baraza hilo simamizi litasimamiwa na mwenyekiti ambaye atateuliwa na Rais na wajibu wake utakuwa ni kutunga sera na maongozi ya kufanikisha utendakazi wa NYS,” akaongeza.

Awali, usimamizi wa shughuli na utendakazi wa NYS ulikuwa chini ya Katiba wa Wizara ya Utumishi wa Umma na Vijana.

Hii ndio maana kashfa ya wizi wa Sh791 milioni ilipotekea katika shirika hilo aliyekuwa Katibu wa wizara hiyo Peter Mangiti ndiye alielekezewa kidole cha lawama na kutiwa mbaroni.

Na katika awamu ya pili ya sakata ya NYS inakisiwa kuwa Sh9 bilioni ziliibiwa au kufujwa aliyekuwa Katibu Lilian Omollo ni miongoni mwa washukiwa 22 walioshtakiwa kwa uovu huo.

Rais Kenyatta pia alitia saini Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ugavi wa Mapato, ya 2018 ambao unapendekeza kuwa fedha kutoka mashirika ya maendeleo ya nje, yatumiwe kwa miradi iliyokusudiwa pekee.

Chini ya sheria ya awali, serikali za kaunti zimekuwa zikieleleza pesa hizo, ambazo aghalabu huwa ni ruzuku, kwa shughuli zisizokusudiwa.

Kiongozi wa taifa pia alitia saini miswada mingine mitatu ambayo ni: Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Afya, 2018, Mswada wa Masoroveya wa Mijengo, 2017, Mswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali, 2018, Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Mashirika ya Akiba na Mikopo (Saccos), 2018 na Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Soko la Hisa 2018.