Michezo

Nyuki watibua mechi ya Makolanders na GASPO KWPL

April 2nd, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

VIHIGA Queens ilivuna alama sita muhimu na kuendelea kutamba kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Kenya (KWPL) wakati mechi baina ya Makolanders na GASPO Women ikitibuka dakika ya 50 baada ya nyuki kuzua taharuki.

Mambo yalienda mrama pale Elizabeth Wambui wa GASPO Women alipoachia kombora iliyogonga mligoti wa lango la wapinzani wao Uwanjani Stima Club Nairobi. Nyuki zilianza kuchomeka katika mligoti huo na kusambaa kote huku zikishambulia wachezaji na kila mtu aliyekuwa eneo hilo na kufanya mchezo huo kuhairishwa.

Vihiga Queens ilisalia kifua mbele kwenye jedwali iliporarua Soccer Queens kwa mabao 6-1 pia kunasa ushindi wa mezani baada ya Kayole Starlets kuingia mitini. Topistar Situma alipiga ‘Hat trick’, Terry Engesha alipiga mbili safi naye Maureen Ater alitinga bao moja.

”Wachezaji wangu hupenda kucheza angalau kusaka magoli mengi ili kujiweka pazuri,” kocha wa Vihiga Queens Alex Alumira alisema. Rachael Mwema alipiga ‘Hat trick,’ huku Mwanalima Adams alitikisa wavu mara moja na kubeba Thika Queens kuchuna magoli 4-2 dhidi ya Mathare United Women.

Nao vigoli Mercy Airo na Bertha Omita kila mmoja alicheka na wavu mara moja na kubeba Kisumu Allstars kuzima Kibera Girls Soccer Academy (KGSA) kwa mabao 2-0.

MATOKEO MENGINE

Vihiga Leeds 1-0 Nyuki Starlets

Wadadia LG 1-0 Soccer Queens

Eldoret Falcons 3-3 Oserian Ladies

Trans-Nzoia Falcons 2-0 Spedag FC

Wadadia LG 2-0 Spedag FC

Nyuki Starlets 0-3 Kibera Girls Soccer Academy (KGSA).

Vihiga Leeds 3-2 Kayole Starlets