Nyuki wavamia na kumuua mzee aliyehudhuria mazishi ya mjukuu

Nyuki wavamia na kumuua mzee aliyehudhuria mazishi ya mjukuu

Na LAWRENCE ONGARO

RUNDO la nyuki lilivuruga mazishi katika kijiji cha Makwa kilichoko Gatundu Kaskazini ambapo mzee mmoja alifariki na kuashiria mwanzo wa msiba mwingine.

Kulingana na wakazi wa kijiji hicho, mhanga Mungai Mburu alikuwa amehudhuria mazishi ya mjukuu wake ambaye baada ya kuzikwa nyuki walivamia mahali hapo na kumshambulia.

Wakazi wa kijiji hicho walikuwa wamehudhuria ibada kabla ya mazishi ambapo mwili wa mjukuu huyo ulisafirishwa hadi eneo la mazishi katika kijiji cha Makwa.

Mjane Bi Wanjiku Mburu amesema wote wawili na mumewe – Mburu – walihudhuria mazishi ya mjukuu wao.

“Sisi wote na wale waliohudhuria mazishi walikaribia hadi kaburini na maombi yalifanywa kama kawaida. Baadaye ndipo kulitokea taharuki ambapo nyuki walivamia eneo hilo kwa kishindo huku kila mmoja akikimbilia usalama wake,” alisema Bi Mburu.

Alisema baadaye katika hali hiyo mumewe aliyekuwa na umri wa miaka 85 alianguka chini baada ya kusukumwa na umati na ndipo alivamiwa na rundo hilo la nyuki.

Katika hali hiyo, wasamaria wema walijaribu kumwokoa ambapo alipelekwa katika hospitali ya Igegania iliyoko eneo la Mang’u, Gatundu Kaskazini.

Alipofika hospitalini alitangazwa kuwa amefariki kutokana na ukosefu wa hewa baada ya nyuki hao kumvamia kichwani na miguuni kwa wingi.

Tukio hilo limewaacha wanakijiji na mshangao mkubwa baada ya mzee wa kijiji aliyeheshimiwa kuaga dunia ghafla.

Bw Lawrence Kariuki ambaye ni mkazi wa kijiji hicho alisema nyuki hao haikujulikana mara moja walikotoka.

“Sisi wakazi wa hapa bado tumeachwa na mshangao kwani hatujaelewa jinsi nyuki hao walivyoweza kuvamia waombolezaji kwa ghafla hivyo,” alisema Bw Kariuki.

Baadhi ya wakazi waliohojiwa walisema tukio kama hilo halijawahi kutokea katika eneo hilo na hiyo ni kama nuksi kwa watu wa kijiji hicho.

“Tungetaka serikali ifanye uchunguzi kubainisha hasa ni jambo lipi lingeweza kusababisha tukio hilo kutendeka, ” alisema Bw Kariuki.

Ilidaiwa baada ya tukio hilo kutendeka, nyuki hao walitoweka wasijulukane walielekea upande upi.

You can share this post!

Limbukeni Brentford wawakaba Liverpool koo ligini

Real Madrid na Villarreal ni nguvu sawa La Liga