Habari Mseto

Nyumba 1,000 sasa zishabomolewa

August 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

TAKRIBAN nusu ya nyumba zilizojengwa karibu na mito zimebomolewa tangu shughuli za ubomoaji zilipoanza Nairobi zaidi ya wiki mbili zilizopita.

Kulingana na msimamizi wa kundi la wahudumu kutoka mashirika mbali mbali ya serikali yanayoendesha shughuli hiyo Bw Julius Wanjau, karibu nyumba 1,000 zimebomolewa.

Nyumba hizo zimebomolewa na watu wa kundi lake, au wakazi, na zilikuwa zimeorodheshwa kati ya nyumba zaidi ya 2,000 ambazo zilikuwa zimejengwa kando ya mito.

“Wengi waliokuwa na nyumba zilizokuwa na maki kwa nyumba zao wamezibomoa, wamefanya kazi yetu kuwa rahisi,” alisema.

Baadhi ya maeneo ambako wamebomoa ni Kileleshwa, Kombo Munyiri na Kiruga, aliongeza na kuelezea kuwa baadhi ya nyumba zilikuwa zimekalia mto.