Nyumba ya gaidi wa Al Shabaab kutwaliwa na serikali

Nyumba ya gaidi wa Al Shabaab kutwaliwa na serikali

Na RICHARD MUNGUTI

NYUMBA ya mwanamke iliyojengwa na fedha za kundi la magaidi wa Al Shabaab jijini Nairobi imetwaliwa na Serikali.

Mbali na kutwaliwa kwa jumba hilo mahakama iliamuru Rose Awinja Ondumbu awekwe chini ya usimamizi wa polisi kwa miaka mitano.

Jumba hilo la kifahari liko eneo la Umoja III karibu na Hospitali ya Mama Lucy, kaunti ya Nairobi. Jumba hilo lilikuwa limekodishiwa mwakilishi wa wadi kaunti ya Machakos tangu 2017. Awinja alijihusisha na usimamizi wa jumba hilo kati ya Desemba 1 2013 na Machi 15,2017.

Akiamuru Awinja awekwe chini ya usimamizi wa polisi na kutwaliwa kwa jumba hilo hakimu mwandamizi Bw Kenneth Cheruiyot alisema masaibu chungu nzima yalimwandama ajuza huyo mwenye umri wa miaka 64. Bw Cheruiyot alisema mwanawe Awinja Anwar Yogan Mwok alijiunga kisiri na kundi la Al Shabaab na kuuawa na wanajeshi wa Kenya (KDF) waliowavamia na kuwashambulia magaidi hao Mogadishu.

Hata hivyo hakimu alimpata na hatia mshtakiwa ya kumiliki na kukodisha mali iliyostawishwa na pesa za kundi la kigaidi la Al Shabaab. Hakimu alisema sheria imesema ikiwa imethibitishwa mali imestawishwa na fedha za kundi la kigaidi litwaliwe na serikali.

Hakimu alisema upande wa mashtaka ulio ongozwa na wakili wa serikali Bw Kibiwott Kiprono ulithibitisha kwamba jumba hilo lililoko Nasra Gardens Estate karibu na Hospitali ya Mama Lucy ilimilikiwa na Anwar Yogan Mwok aliyeuawa wakati wa makabiliano makali na maafisa wa KDF mnamo 2017.

“Hii mahakama imechambua na kuzingatia ushahidi wote uliowasilishwa na upande wa mashtaka na kufikia uamuzi Awinja yuko na hatia ya kusimamia na kupokea pesa kutoka kwa jumba la gaidi wa Al Shabaab,” alisema Bw Cheruiyot.

Hata hivyo hakimu alifutilia mbali shtaka Awinja kutuma pesa kwa kundi hilo la Al Shabaab kutokana na ada ya kukodishwa kwa jumba hilo. Akiomba mahakama imwonee huruma wakati wa kupitisha adhabu, Awinja alisema hakujua mwanawe alikuwa amegeuka kuwa gaidi kwa vile alimweleza aliajiriwa kazi Somali na shirika moja la kimataifa.

Awinja alieleza korti alifahamishwa kuwa mwanawe ni gaidi alipouawa na maafisa wa KDF. Punde tu baada ya habari kuenea Mwok alikuwa gaidi, mkewe na mwanawe walitoroka na kumwacha mshtakiwa peke yake akiugua huku uzee ukimkaba kabisa.

“Naomba hii mahakama inioneee huruma kwa vile mimi sina mbele wala nyuma. Mwanangu aliuawa Somalia. Mkewe alitoroka na mjukuu wangu. Nimesalia pweke na mgonjwa.Uzee nao umebisha kwa kasi,” Awinja alimrai hakimu.

Mahakama iliombwa na wakili John Khaminwa ambaye alikuwa mahakamani imwonee huruma Awinja anayeugua na mwili wake umedhoofika. Akipitisha hukumu hakimu alisema , “ Hii mahakama imetilia maanani wewe humgojwa na hauna mtu wa kukutunza. Kukupeleka jena miaka 20 au zaidi ni sawa na kupitisha adhabu ya kifo dhidi yako.”

Hatimaye aliagizwa awe chini ya uangalizi wa polisi kwa miaka mitano. Kesi hiyo itatajwa tena Desemba 16,2021 kwa maagizo zaidi.

You can share this post!

Wakufunzi zaidi ya 400 wameshtaki vyuo vikuu viwili kwa...

Mlofa mwizi ajuta baada ya simu kuita jina la mwenyewe

T L