Nyundo ya West Ham United yazamisha Chelsea ligini

Nyundo ya West Ham United yazamisha Chelsea ligini

Na MASHIRIKA

WEST Ham United waliweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kunogesha kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao wa 2022-23.

Hii ni baada ya kikosi hicho cha kocha David Moyes kutoka nyuma mara mbili na kuduwaza miamba Chelsea kwa kichapo cha 3-2 ugani London, Jumamosi.

Manuel Lanzini, Jarrod Bowen na Arthur Masuaku walifunga mabao ya West Ham huku Chelsea ya mkufunzi Thomas Tuchel wakipata magoli yao kupitia Thiago Silva na Mason Mount.

West Ham kwa sasa wameshinda mechi nane, kuambulia sare mara tatu na kupoteza michuano minne kati ya 15 iliyopita. Matokeo hayo yanawadumisha katika nafasi ya nne jedwalini kwa alama 27, sita pekee nyuma ya Chelsea ambao ni wafalme wa UEFA.

Ni pengo la pointi nne ndilo linatenganisha West Ham na Arsenal watakaokuwa wageni wa Everton hapo kesho ugani Goodison Park.

Ushindi dhidi ya Chelsea ulikomesha rekodi duni ya West Ham ambao hawakuwa wameshinda mechi tatu mfululizo za awali ligini tangu wacharaze Liverpool 3-2 mnamo Novemba 7.

Kushindwa kwa Chelsea kunawaweka katika presha zaidi kadri wanavyojitahidi kuhimili ushindani mkali kutoka kwa mabingwa watetezi Manchester City na Liverpool ambao pia ni miongoni mwa wagombezi halisi wa ubingwa wa EPL msimu huu.

Baada ya kuvaana na Zenit St Petersburg ya Urusi katika mechi ya mwisho ya makundi ya UEFA wiki ijayo, Chelsea watakuwa na kibarua kizito ligini dhidi ya Leeds United, Everton na Wolves. Watamenyana baadaye na Brentford kwenye robo-fainali za Carabao Cup kabla ya kukamilisha kampeni zao za EPL mnamo Disemba dhidi ya Aston Villa na Brighton mtawalia.

Kwa upande wao, West Ham watakuwa wenyeji wa Dinamo Zagreb ya Croatia kwenye Europa League Alhamisi ijayo kabla ya kupepetana na Burnley, Arsenal na Norwich City kwa usanjari huo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Shujaa yapigwa na Great Britain kumaliza raga ya Dubai 7s...

Shirika la PrimRose laokoa walevi Gatundu Kaskazini

T L