Nzamba Kitonga aombolezwa kama shujaa

Nzamba Kitonga aombolezwa kama shujaa

Na BENSON MATHEKA

WAKILI Nzamba Kitonga aliyefariki Jumamosi baada ya kuugua ghafla, ametajwa kuwa mwansheria shupavu katika masuala ya kikatiba, na mzalendo aliyejitolea kufanya Kenya kuwa nchi bora.

Mwili wa Bw Kitonga ambaye aliongoza kamati ya wataalamu walioandika Katiba iliyopitishwa na Wakenya 2010 (COE), ulihamishiwa mochari ya Lee jijini Nairobi kutoka Machakos alikofariki akipokea matibabu.

Viongozi walisema kifo chake ni pigo kwa nchi wakati huu ambapo juhudi za kubadilisha katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) zinaendelea.

Rais Uhuru Kenyatta alimtaja marehemu Kitonga kama rafiki yake ambaye mchango wake katika huduma kwa umma umenakiliwa vilivyo katika historia ya Kenya.

‘Nimehuzunishwa sana na kifo cha ghafla cha rafiki yangu mwanasheria Nzamba Kitonga, mwanasheria stadi wa masuala ya kikatiba na kiongozi ambaye ufanisi wake katika huduma ya umma umenakiliwa vilivyo.”

Kwenye risala yake kwa familia na wanasheria, Rais Kenyatta alisema mchango wa wakili huyo katika kuunda katiba utamfanya akumbukwe daima.

Rais Mstaafu Mwai Kibaki alisema kifo cha Nzamba ni pigo kwa mahakama na Kenya kwa jumula. Alisema marehemu alihudumu kwa kujitolea bila kuogopa chochote.

“Atakumbukwa kwa mchango wake katika kufanikisha katiba ya Kenya ya 2010 ambayo ilikamilisha juhudi za miaka mingi za kubadilisha katiba,” Bw Kibaki alisema kwenye taarifa.

“Ustadi wa Nzamba kama kiongozi wa kundi la wataalamu ulisaidia Kenya wakati muhimu wa mpito ambao Kenya iliacha kutumia katiba iliyokuwa nayo tangu uhuru,” alisema.

Ni Kibaki aliyemteua Nzamba kusimamia kundi la wataalamu walioandika katiba iliyopitishwa 2010.Naibu Rais William Ruto alimtaja Nzamba kama kiongozi aliyekuwa na kipawa cha kuona mbali.

Dkt Ruto alikuwa miongoni mwa waliopinga katiba ya 2010 ambayo kamati ya wataalamu iliyoongozwa na Nzamba iliandika.Naye aliyekuwa waziri mkuu wakati kamati ya Nzamba ilipoandika katiba, Bw Raila Odinga, alisema Kenya imempoteza wakili wa hadhi ya juu, na shujaa wa masuala ya katiba.

“Dkt Kitonga alikuwa akifasiri katiba kuhakikisha imelingana vyema na watu wetu na nchi yetu,” Bw Odinga alisema.

“Kifo chake ni pigo kwa juhudi zetu za kuimarisha katiba ya 2010 ambayo aliandika akiwa mwenyekiti wa kamati ya wataalamu,” aliongeza Bw Odinga.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM anashinikiza katiba hiyo kurekebishwa kupitia mchakato wa Maridhiano (BBI) alioanzisha akiwa na Rais Kenyatta.

Katika risala yake, Jaji Mkuu David Maraga alimwomboleza marehemu kama nguzo ya safari ya katiba ya Kenya. “Alikuwa mmoja wa wanasheria walioheshimiwa na nguzo ya kutegemewa katika safari ya katiba ya nchi hii,” alisema.

Kulingana na mwenyekiti wa chama cha wanasheria nchini (LSK), Nelson Havi, kifo cha ghafla cha Bw Kitonga ni pigo kwa taaluma ya uanasheria nchini.

Marehemu, aliyekuwa na umri wa miaka 64, aliugua akihudhuria mazishi katika Kaunti ya Kitui na alifariki akipelekwa hospitalini Nairobi.

Amewahi kuwa mwenyekiti wa chama cha wanasheria nchini na chama cha mawakili cha Afrika Mashariki. Aidha, amewahi kuhudumu kama jaji wa mahakama ya haki ya Afrika Mashariki na Kusini.

Alikufa siku moja baada ya kuwaandalia karamu jamaa wa karibu wa familia yake nyumbani kwake Mutito, Kaunti ya Kitui.

You can share this post!

Aliyemuua mjombake auawa na wakazi

Corona yamuua muuguzi Mombasa