Habari Mseto

Nzige: Viongozi wataka wakulima walipwe fidia

February 10th, 2020 2 min read

STANLEY NGOTHO, ALEX NJERU na VALENTINE OBARA

VIONGOZI wa Kaunti ya Tharaka-Nithi wakiongozwa na Seneta Kithure Kindiki na Mbunge wa Tharaka, Bw Gitonga Murugara wanaitaka serikali kuu kuwalipa fidia wakulima wote ambao mimea yao imeharibiwa na nzige.

Jana, wakulima katika eneobunge la Tharaka na sehemu za Kaunti ya Kajiado walihofia hasara kubwa na njaa baada ya nzige kuvamia mashamba yao.

Awali nzige walikuwa wamevamia vijiji vya Kaunti Ndogo ya Tharaka Kaskazini lakini jana wakawa wameenea katika karibu eneobunge zima la Tharaka.

Tayari wameharibu mamia ya hekta ya mashamba ya wimbi, mtama, pojo, mahindi miongoni mwa mimea mingine.

Akizungumza jana wakati alipozuru mashamba yaliyovamiwa Tharaka Kaskazini, Prof Kindiki alisema serikali inafaa ichukulie suala la nzige kwa uzito zaidi la sivyo kutakuwa na janga kuu la njaa.

“Binadamu na mifugo imebaki bila chochote cha kukula katika eneobunge la Tharaka na sehemu zingine nyingi za nchi,” akasema.

Serikali imekuwa ikikumbwa na changamoto ya dawa za kutosha kuangamiza wadudu hao, kwani lazima ziagizwe kutoka Japan.

Bw Murugara alisema nzige tayari wametaga mamilioni ya mayai na yasipoharibiwa, kutakuwa na janga baadaye.

Katika Kaunti ya Kajiado, maafisa wa kilimo walisema nzige walivamia wadi za Malilima, Dalalekutuk, na Kikuro katika eneo la Kajiado ya Kati.

Maeneo mengine yaliyoathirika ni Kajiado Mashariki na Kajiado Kusini.

Waziri wa Kilimo na Mifugo katika kaunti hiyo, Bi Jackline Koin alithibitisha kwamba maafisa wameripoti wadudu hao wanaharibu mimea yote.

Kufikia sasa, Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) linalosimamiwa na Umoja wa Mataifa limeripoti nzige wameonekana katika kaunti 14 nchini na wanaendelea kuenea.

Kaunti nyingine zilizoshambuliwa majuzi ni Narok, Makueni, Machakos, Kitui na Taita Taveta.

Katika mkutano ulioandaliwa na FAO jijini Addis Ababa, Ethiopia mnamo Ijumaa, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Bi Maria Helena Semedo alisema ni muhimu nzige waangamizwe kwa haraka.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wawakilishi wa mataifa yaliyoathirika kufikia sasa yakiwemo Kenya, Ethiopia na Somalia, huku kukiwa na tahadhari kwamba huenda wadudu hao wakaingia Sudan Kusini na Uganda hivi karibuni.

“Nzige huwa hawasubiri. Wao huenda mahali popote wanapotaka na kuharibu chochote kile wanachotaka. Tafadhalini msisubiri kabla kuchukua hatua, tushirikiane pamoja ili kuimarisha oparesheni zetu na juhudi za kutudishia umma hali yao ya kawaida ya kimaisha,” akasema.

Katika mkutano huo, wadau walikubaliana kutafuta mbinu mpya za kukabiliana na wadudu hao waharibifu katika nchi zao.

Humu nchini, serikali imekuwa ikinyunyiza dawa kutoka hewani katika baadhi ya maeneo ili kuwaangamiza nzige, ingawa wadudu hao walikuwa wangali wanaenea hadi maeneo mapya kufikia jana na hivyo kuibua maswali kuhusu kama mbinu zinazotumiwa na serikali zinafaulu.