Habari Mseto

Nzige wavamia mashamba na malisho Lamu

December 3rd, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

BAA la njaa linawakodolea macho wakazi wa Kaunti ya Lamu kufuatia nzige waharibifu kuvamia mashamba yao kwa mara ya kwanza juma hili.

Nzige hao wameharibu mimea katika vijiji vya Mararani, Mangai, Mswakini, Bar’goni, Poromoko, Miruji, Kitumbini, Pandanguo, Maleli, Moa, Mpeketoni, Katsaka Kairu, Boramoyo, Zebra na Hindi.

Wakulima waliozungumza na Taifa Leo Alhamisi walieleza hofu ya kukosa mazao msimu huu baada ya nzige kuharibu mimea yote mashambani.

Mutua Kitetu ambaye ni mkulima wa mahindi, mtama, pojo na maharagwe eneo la Miruji, tarafa ya Mpeketoni, alisema ekari zake nne za mimea zote zimefyekwa na nzige hao tangu walipovamia mashamba yao mapema juma hili.

Bw Kitetu aliiomba serikali kuingilia kati na kuwapulizia dawa wadudu hao na pia kuharibu mayai yao kabla hayajaanguliwa na kuongeza mamilioni ya nzige zaidi eneo hilo.

“Mamia ya ekari za mashamba yetu tayari yameharibiwa na hao wadudu hatari; mimi binafsi nikipoteza ekari nne za mimea yangu iliyofyekwa na nzige,” akasema Bw Kitetu.

Kamau Mbuthia ambaye ni mkulima eneo la Mpeketoni aliiomba serikali na wadau kujitokeza ili kuwasaidia wakulima kupambana na janga la nzige.

Bw Mbuthia pia aliiomba serikali kufikiria kuwafadhili wakulima kwa mbegu za kisasa ili wapande upya baada ya mimea yao kuharibiwa na wadudu hao ambao kwa sasa bado wanaendeleza uharibifu mashambani mwao.

“Watusaidie kunyunyiza dawa za kuua nzige na mayai yao. Kisha wafikirie kuwafadhili wakulima kwa mbegu ili tupande upya. Hali si nzuri mashambani mwetu kwa sasa,” akasema Bw Mbuthia.

Salim Abdi ambaye ni mfugaji wa kuhamahama pia alieleza wasiwasi kwamba ikiwa tatizo la nzige halitakabiliwa na kumalizwa eneo hilo, huenda wafugaji pia wakakosa sehemu za kulishia ng’ombe, mbuzi na kondoo wao.

Alisema tangu juma lilipoanza, mamilioni ya nzige wamekuwa wakionekana kwenye maeneo yao ya malisho wakiendeleza uharibifu.

“Wadudu hao wanaotembea kwa makundi pia wamevamia sehemu zetu za malisho wakiendeleza uharibifu,” akasema Bw Salim.

Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Irungu Macharia, alithibitisha kuwa sehemu nyingi za Kaunti ya Lamu zimeathirika na nzige.

Bw Macharia alisema maeneo yote yaliyovamiwa na wadudu hao ndiyo uti wa mgongo kwa kilimo cha Lamu, hatua ambayo alisema huenda ikaathiri pakubwa utoshelezaji na usalama wa chakula eneo hilo.

Alisema serikali kuu kwa ushirikiano na ile ya kaunti tayari wameanzisha shughuli ya kusambaza kemikali za kunyunyizia na kuua nzige pamoja na mayai yao.

Alisema shughuli ya kuwaelimisha wakulima kuhusu mbinu za kukabiliana na kuwamaliza nzige mashambani pia zinaendelea kwenye maeneo mbalimbali ya Lamu.

“Nzige hao tunaamini walivuka Lamu kupitia Hulugho ambao ni mpaka wa Lamu na Garissa na walianza kwa kuvamia mashamba ya Mangai, Mararani, Mswakini na Bar’goni kabla ya kusambaa kote Lamu. Serikali ya kitaifa tayari inaendeleza usambazaji wa kemikali ya kuua wadudu hao waharibifu. Pia tunashirikiana na kaunti ili kuwaelimisha wakulima jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo,” akasema Bw Macharia.