Michezo

Nzoia Sugar FC yasalia bila ushindi kwenye Ligi Kuu

September 14th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Nzoia Sugar FC wamesalia bila ushindi kwenye Ligi Kuu ya msimu huu baada ya kupoteza penalti wakichapwa 2-1 na SoNy Sugar uwanjani Sudi mjini Bungoma, Jumamosi.

Nzoia ilipata penalti dakika ya 32, lakini kipa akaipangua.

Stephen Onyango alifungulia SoNy akaunti ya magopli dakika nane baadaye kabla ya Salmon Omollo kufanya mambo kuwa 2-0 dakika ya 65. Brian Wepo alifungia Nzoia bao la kufutia machozi dakika ya 82.

Katika mechi iliyotangulia kusakatwa uwanjani Kenyatta, mabingwa wa zamani Tusker na Mathare United waligawana alama katika sare ya 1-1.

Timothy Otieno aliweka Tusker mbele 1-0 kupitia penalti dakika ya 71 kabla ya Klinsman Omulanga kusawazisha zikisalia sekunde chache kipenga cha mwisho kilie.

Mechi kati ya mabingwa wa zamani Ulinzi Stars na Sofapaka ilitamatika 0-0 uwanjani Afraha, huku Western Stima pia ikiandikisha matokeo sawa na hayo uwanjani Moi mjini Kisumu dhidi ya Wazito.

Nayo Posta Rangers ilitoka nyuma na kugawana alama katika sare ya 1-1 dhidi ya Kakamega Homeboyz katika mechi ya pili ya siku uwanjani Machakos.

Wageni Homeboyz walichukua uongozi kupitia kwa Peter Thiong’o aliyemegewa pasi na Allan Wanga kabla ya Rangers kupokonya klabu hiyo kutoka kaunti ya Kakamega ushindi kinywani dakika ya 88.