Habari MsetoSiasa

Obado akimbizwa hospitalini baada ya kulemewa na maisha ya seli

October 3rd, 2018 1 min read

Na WANDERI KAMAU

GAVANA wa Migori, Okoth Obado Jumatano alikimbizwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) baada ya kulalamikia matatizo ya tumbo akiwa rumande katika gereza la Industrial Area, jijini Nairobi.

Duru katika hospitali hiyo zilisema kuwa Bw Obado alilazwa katika wadi ya kibinafsi mwendo wa saa sita adhuhuri, ili kupata matibabu maalum.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Matibabu katika hospitali hiyo Dkt Peter Masinde, alithibitisha kulazwa kwa gavana huyo lakini akasema hali yake ilikuwa shwari.

“Ni kweli kwamba amelazwa lakini hali yake si mbaya,” akasema Dkt Masinde.

Baada ya kushughulikiwa katika wadi maalum, gavana huyo alilazwa katika wadi ya kawaida, japo chini ya ulinzi mkali na kufichwa.

Muuguzi mmoja ambaye hakutaka kutajwa, alisema kuwa Bw Obado alihamishiwa katika wadi hiyo ya kawaida mwendo wa saa tisa alasiri.

Wakati Taifa Leo ilipozuru hospitali hiyo jana alasiri, hali ya usalama ilikuwa kali, huku wadi alimolazwa ikiwa chini ya ulinzi wa polisi waliojihami.

Polisi hao pia walikuwa wakishika doria nje ya hospitali hiyo.

Wale waliokuwa na wagonjwa wao katika wadi zilizo karibu na aliyolazwa Bw Obado walilazimika kujitambulisha na kufanyiwa ukaguzi maalum na walinzi kwa ushirikiano na polisi kabla ya kuruhusiwa kuingia.

Bw Obado amekuwa rumande kwa wiki mbili sasa baada ya kunyimwa dhamana na mahakama kuhusiana na mashtaka yanayomkabili ya mauaji ya mwanafunzi Sharon Otieno, wa Chuo Kikuu cha Rongo.

Gavana huyo anatarajiwa mahakamani Jumatatu wiki ijayo.