HabariSiasa

OBADO ANYONGWE – DPP

October 13th, 2018 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

OFISI ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji Ijumaa iliambia mahakama kuu ataomba adhabu ya kifo ipitishwe dhidi ya Gavana wa Migori Okoth Obado huku akiamriwa azuiliwe gerezani kwa siku 12 kabla ya ombi lake la dhamana kuamuliwa.

Jaji Jessie Lesiit aliamuru Bw Obado, aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na karani wa kaunti Bw Caspal Obiero wataendelea kuzuiliwa katika gereza la Viwandani hadi Oktoba 24, 2018 atakapoamua ikiwa atamwachilia kwa dhamana au la.

Washtakiwa hawa waliomba waachiliwe kwa dhamana wakisema “ni haki yao ya kikatiba na hakuna ushahidi kwamba walivuruga mashahidi na kuwatisha.”

Mawakili wa Bw Obado wakisoma stakabadhi wakati kesi ilikuwa inaendelea Oktoba 12, 2018. Picha/ Richard Munguti

Offisi ya DPP ilipinga wakiachiliwa ikisema yuko na ushahidi wa kutosha kuthibitisha watatu hao walihusika na mauaji ya mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Rongo Sharon Otieno na mtoto wake Baby Sharon.

Naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Jacob Ondari aliambia Jaji Lesiit, “nitaomba adhabu ya kifo ipitishwe dhidi ya washtakiwa hawa.”

Bw Ondari alisema atawaita mashahidi 24 watakaothibitisha mashtaka dhidi ya Gavana Obado, Oyamo na Obiero aliosema ndio wa kwanza kushtakiwa kwa mauaji ya mtoto ambaye hajazaliwa.

“Mashtaka dhidi ya washtakiwa hawa ni mabaya kwa vile wameshtakiwa kumuua Baby Sharon na mama yake-Sharon Beylne Itieno,” Bw Ondari.

Mmoja wa mawakili ampa mkono wa kumtia moyo Gavana Obado mahakamani. Picha/ Richard Munguti

Bw Ondari alisema adhabu ya kifo inayowakondolea macho washtakiwa ni kishawishi cha washtakiwa  kutoroka wakiachiliwa kwa dhamana.

“Ijapokuwa Mahakama ya Juu imetoa ushauri kuhusu adhabu ya kifo, bado sheria hiyo ingali katika vitabu vya sheria vya humu nchini. Nitaomba mahakama ipitishe adhabu hiyo ya kifo hatimaye,” alisema Bw Ondari.

Mahakama iliambiwa iendelee kumzuia Bw Obado gerezani kwa vile atawavuruga mashahidi na kuwatisha wasifike kortini.

Korti iliambiwa Obado yuko na ushawishi mkubwa Migori na mashahidi wataogopa kufika kortini kutoa ushahidi dhidi yake.

Mabw Ondari na Muteti walimweleza Jaji Lesiit kuwa ijapokuwa dhamana inakubaliwa katika Katiba Kifungu nambari 49 korti inaweza kuwanyima washtakiwa kwa misingi ya maslahi ya umma.

Wawili hao walieleza korti sababu ya kuwa na mke na watoto sio sababu ya kuachiliwa kwa dhamana.

Aliyekuwa msaidizi wa Bw Obado, Michael Oyamo afunguliwa pingu wakati walifikishwa mahakamani. Picha/ Richard Munguti

Kiongozi huyo wa mashtaka alisema mawakili wanaowatetea washtakiwa hawajui wanalopenda kwa vile waliomba korti ikabidhiwe ushahidi wa ulionukuliwa kutoka kwa mashahidi ndipo wautengemee kuwasilisha ombi.

“ Mawakili wa washtakiwa wamekabidhiwa nakala za mashahidi na sasa hawataki ukizingatiwa katika uamuzi wa ombi hili la dhamana,” alisema Bw Ondari.

Jaji huyo alifahamishwa na viongozi hao wa mashtaka hakuna siasa zozote kwenye kesi hii mbali kile kinategemewa sheria na ushahidi uliopo.

Bw Ondari alisema dhana kuwa washukiwa walitekeleza mauaji ni sababu tosha ya kuwanyima dhamana. “Mkenya anaweza kunyimwa dhamana kwa tuhuma aliua,” Bw Ondari.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa wakiongozwa na Jaji (mstaafu) Nicholas Ombija , Cliff Ombeta , Rogers Sagana, Neville Amolo na wengine saba walilalamika DPP ametegemea ushahidi wa mashahidi kupinga washukiwa wakiachiliwa kwa dhamana.

Bw Obado na wakili wake Cliff Ombeta baada ya korti kuamuru azuiliwe kwa siku 12 zaidi. Picha/ Richard Munguti

Walisema hakuna sababu zozote ziliwasilishwa na DPP kuthibitisha washtakiwa watavuruga mashahidi na kwamba walitoa vitisho kwa mashahidi.

“Hakuna hata shahidi mmoja kati ya 24 walioandikisha ushahidi hakuna aliyesema alitishwa aidha na Obado, Oyamo ama Obiero,” Bw Ombeta alisema

Walisema maisha ya washtakiwa hayamo hatarini kama inavyodaiwa na DPP.

Bw Ombeta alisema serikali inapasa kuwalinda washtakiwa na kamwe haipasi kusemwa eti wanatishiwa maisha.

Aliomba ushahidi wa mama wa Sharon utupwe na ule wa afisa anayechunguza kesi hiyo Clement Mwangi akisema unafichua ushahidi ambao haujatolewa kortini.

Bw Obado arudishwa katika seli ya Viwandani. Picha/ Richard Munguti

Mawakili hao walisema kifungu nambari 49 chaitaka korti kuachilia kila mshukiwa kwa dhamana.

Mabw Ombeta , Omollo, Jaji Ombija na Sagana waliambia mahakama kuwa katiba ndiyo sheria kuu ya nchi na kwamba jukumu kuu la majaji na mahakimu ni kuitekeleza.

“Naomba hii mahakama ijinasue na kasumba ya katiba ya zamani iliyofanya hii mahakama ionekane kama idara ya kukandamiza haki za washukiwa,” Jaji Ombija.

Jaji huyo wa zamani alimsihi Jaji Lesiit azingatie vifungu nambari 20 na 25 vya katiba vinavyohimiza kuzingatiwa kwa haki za binadamu.