Habari MsetoSiasa

Obado azongwa na shinikizo jipya la kumng’oa mamlakani

November 2nd, 2018 2 min read

Na DAVID MWERE

MASAIBU ya Gavana wa Migori Okoth Obado yameongezeka baada ya shirika moja lisilo la kiserikali kushinikiza kuondolewa kwake afisini kutokana na mauaji ya mwanafunzi Sharon Otieno na ufujaji wa fedha za umma.

Pamoja na wengine, Bw Obado ameshtakiwa kwa mauaji ya Bi Otieno, aliyekuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Rongo na mtoto wake ambaye hakuwa amezaliwa.

Na ijapokuwa aliachiliwa kwa dhamana, washukiwa wenzake wangali wanazuiliwa.

Bw Obado pia anakabiliwa na kesi ya ufujaji wa fedha za umma, hali ambayo imefanya akaunti zake za benki kufungwa.

Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) tayari imefunga akaunti za jamaa na washirika wake wa karibu kwa madai ya uporaji wa zaidi ya Sh2 bilioni kutoka kwa serikali ya kaunti hiyo.

Kwenye malalamishi iliyowasilisha kwa EACC, Kituo cha Kimataifa cha Sera na Kukabiliana na Migogoro (ICPC) kinaitaka tume hiyo kumshinikiza gavana huyo kuondoka afisini kwa madai ya kukiuka Kipengele cha Sita Kuhusu Maadili. Kinamtaka gavana kuondolewa kwa nguvu au kushinikizwa kujiuzulu.

“Kesi ya Obado inatoa nafasi kwa EACC kudhihirisha kujitolea kwake kukabiliana na ukiukaji wa sheria miongoni mwa maafisa wakuu wa serikali. Lazima juhudi hizo ziwiane na vita vinavyoendelea dhidi ya maovu yaliyotaasisika serikalini,” akasema Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Ndung’u Wainaina.

“Katiba inamhitaji anayeshikilia afisi yoyote ile ya umma kuwa na kiwango cha juu cha uadilifu, kama ilivyo kwa taasisi anayoshikiliia,” akasema Bw Wainaina.

Kulingana na Bw Wainaina, hali ya viongozi wasio waadilifu kuendelea kushikilia afisi hizo kunaziharibia sifa.

Mkurugenzi huyo anashikilia kuwa kesi hizo mbili zinazomkabili Bw Obado zimetoa sababu kuu kwa kiongozi huyo kuondolewa afisini, chini ya kipengele 181 (1) cha Katiba.

Kulingana na kipengele hicho, sababu kuu ambazo kiongozi anaweza kuondolewa afisini ni ukiukaji wa katiba, matumizi mabaya ya mamlaka au matatizo ya kiakili ambayo yanamzuia kutekeleza majukumu yake ifaavyo.

Mkurugenzi huyo alinukuu uamuzi wa Jaji JB Ojwang’ kuhusu aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu Nancy Baraza, ambapo aliondolewa afisini kwa kumshambulia mlinzi mmoja. Kulingana naye, kuna sababu za kutoshaza kisheria kumshinikiza gavana huyo kuondoka afisini.

“Bw Obado haaminiwi tena na umma, kutokana na mashtaka yanayomkabili. Ni kinaya kwake kuendelea kuwaongoza watu ambao hawamwamini kama kiongozi wao,” akasema.

Bw Wainaina anaamini kuwa kuna haja kubwa kuwazuia watu ambao wanakabiliwa na tuhuma za uhalifu kutoshikilia afisi yoyote ya umma.