Obado na watoto wake wanne kujibu mashtaka ya ufisadi wa Sh73.4M

Obado na watoto wake wanne kujibu mashtaka ya ufisadi wa Sh73.4M

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Migori Okoth Obado na watoto wake wanne na washtakiwa wengine 10 watajibu mashtaka upya Alhamisi (oktoba 21) kwa ulaghai na ufujaji wa zaidi ya Sh73milioni.

Uamuzi wa kuwashtaki upya Obado ulifuatia kutupiliwa mbali kwa ombi lake la kupinga cheti cha mashtaka kilichotayarishwa na Polisi.

Hakimu mkuu Lawrence Mugambi anayesikiza kesi hiyo alikataa ombi la Bw Obado akisema,“sikubaliani na mawasilisho kuwa mkurugenzi wa mashtaka ya umma –DPP Noordin Haji- hakutayarisha mashtaka mwenyewe mbali aliachia polisi watekeleze majukumu yake.”

Katika uamuzi aliotoa Bw Mugambi alisema malalamiko ya Bw Obado kwamba sio Bw Haji aliandaa na kutayarisha cheti cha mashtaka kulingana na sheria iliyopitishwa miaka 11 iliyopita hayana mashiko kisheria.

Bw Mugambi alisema nukuu za Katiba ambazo wakili mwenye tajriba ya juu Kioko Kilukumi alimsihi azingatie kukataa mashtaka hayo mapya haziwezi kumfaa Obado. “Vile nilivyoruhusu ushahidi mpya uwasilishwe wakati huo huo niliruhusu nakala ya mashtaka yaliyoambatanishwa,” akasema Bw Mugambi.

Hakimu huyo alisema, kiongozi wa mashtaka  Bi Hellen Mutellah alithibitisha sheria zilizopendekezwa miaka11 hajizaanza kutekelezwa.“Sheria za kutaka afisi ya ODPP iwe ikitayarisha cheti cha mashtaka badala ya polisi zimo katika harakati ya kuzinduliwa na bado hazijaanza kutekelezwa,” alisema Bi Mutellah.

Aliomba korti ikubalie mashtaka yaliyotayarishwa na polisi na kupigwa muhuri na afisi ya ODPP na pia kupokewa na idara ya mahakama. Wakili Kilukumi alieleza mahakama “daftari ya mashtaka yaliyowasilishwa na Polisi sio mashtaka halisi.”

Aliomba korti iyafutilie mbali. Mawakili wengine George Kithi na Collins Ario waliomba korti ikatae mashtaka hayo.Hakimu alikubaliana na Bi Mutellah na kusema polisi ndio walichunguza kesi na hatimaye wakaandaa cheti cha mashtaka kilichopigwa chapa na afisi ya ODPP.

Alisema cheti hicho cha mashtaka kimewasilishwa kwa mujibu wa sheria. Obado ameshtakiwa pamoja na watoto wake Susan Scarlet, Jerry Zachary, Evelyn Adhiambo na Dan Achola Okoth. Washtakiwa wengine ni pamoja na Bw Jared Kwaga anayeshtakiwa pamoja na mkewe na mama yao.

  • Tags

You can share this post!

Watu 26 wanaoishi na ulemavu Kiambu wapokea vifaa vya kazi...

NGILA: Tumia ufadhili wa Google kupiga jeki biashara yako

T L