Habari MsetoSiasa

Obado sasa alazimika kuhama nyumbani

October 29th, 2018 1 min read

 Na ELISHA OTIENO

GAVANA wa Migori Okoth Obado sasa amehamia nyumba yake ya zamani iliyoko Kaunti ya Migori kutii agizo la mahakama kwamba anafaa kuishi kilomita 20 kutoka mpaka wa Kaunti ya Homa Bay.

Nyumba yake ya kifahari iliyoko eneo la Rapogi katika Kaunti Ndogo ya Uriri inapatikana kilomita 15 kutoka mpaka wa Kaunti ya Migori na Homa Bay, ambako aliyekuwa mpenzi wake Sharon Otieno aliuawa.

Bidhaa za kibinafsi za gavana huyo zikiwemo nguo zilitolewa boma lake la Rapogi punde tu alipowasili Migori kutoka Nairobi mnamo Jumamosi.

Nyumba anayoishi Migori inamilikiwa na kampuni ya BAT Kenya na ilikodishwa na serikali ya kaunti mnamo 2014.

Bw Obado alihama nyumba hiyo miaka mitatu iliyopita ujenzi wa nyumba yake ya mashambani ulipokamilika na amekuwa akihudumu kutoka Rapogi.

“Tunaheshimu masharti yaliyowekwa na mahakama ingawa yametutatiza. Bw Obado sasa atakuwa akihudumu kutoka hapa,” alisema msaidizi wake mmoja ambaye aliomba tusitaje jina lake.

Bw Obado aliachiliwa kwa dhamana wiki iliyopika kwenye kesi ya mauaji ya Sharon.

Ameshtakiwa pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa karani mkuu wa kaunti hiyo Bw Caspar Obiero.