Bambika

Obama amwaga jumbe za kumsifia mkewe

January 19th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MKEWE aliyekuwa Rais wa 44 wa Amerika, Barack Obama, Michelle Obama, alifikisha umri wa miaka 60 tangu kuzaliwa kwake mnamo Jumatano.

Kama njia ya kumwonyesha mapenzi ya kipekee siku yake ya kuzaliwa, Obama alimwandikia ujumbe wa kimapenzi kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), akimtakia maisha marefu yaliyojawa na neema za Mungu.

“Hivi ndivyo mtu huwa anakaa akifikisha umri wa miaka 60. Heri njema siku ya kuzaliwa mpenzi wangu—ambapo wewe ni mtu mwenye ucheshi, werevu na urembo zaidi machoni mwangu. Michelle Obama, huwa unanichangamsha kila siku. Niko tayari sana kuona jinsi miaka kumi ijayo itakuletea,” akasema.

Wawili hao walioana mnamo Oktoba 3, 1992, na wana mabinti wawili.

Mabinti hao ni Malia (aliyezaliwa 1998) na Natasha (anayejulikana pia kama Sasha—aliyezaliwa 2001).

Wawili hao walikutana mnamo 1989 wakati Michelle alipewa jukumu la kumfunza na kumwelekeza Obama kwenye mahakama moja jijini Chicago.

Wakati huo, Obama alikuwa na umri wa miaka 28 huku Michelle akiwa na umri wa miaka 25. Kwenye wasifu wake ‘A Promised Land’ (Nchi ya Ahadi), Obama alisema: “Michelle alinizuzua kimapenzi mara ya kwanza nilipomuona”.

Imekuwa kawaida kwa wawili hao kuonyeshana mapenzi motomoto hadharani na kwenye jumbe ambazo wamekuwa wakiandikiana katika mitandao ya kijamii.

Obama aliongoza Amerika kati ya 2009 na 2017.