OBARA: Badala ya mabomu, tulichagua ufisadi kujiangamiza!

OBARA: Badala ya mabomu, tulichagua ufisadi kujiangamiza!

Na VALENTINE OBARA

KILA tunapowaza au kujadiliana kuhusu mataifa yanayokumbwa na vita, tunajichukulia kama taifa lililobahatika kufurahia amani na utulivu.

Tunafurahia uhuru wa kufanya mengi ambayo wenzetu walio katika mataifa yenye vita hutamani tu.

Tunaweza kusafiri tutakavyo, tunaendeleza biashara zetu mbalimbali, tunaabudu tupendavyo, watoto wetu huenda shuleni na wanapougua wanapata matibabu bora ikilinganishwa na nchi nyingi ulimwenguni.

Kutokana na hali hiyo, wengi wetu huona kila kitu ni shwari.

Lakini tukifumbua macho yetu na kutazama kwa kina yale yanayoendelea katika taifa hili, utakuta kwamba, kwa mauaji, hatuhitaji milio ya risasi na milipuko ya bomu ili tuwe sawa au kukaribia zile nchi zinazokumbwa na machafuko.

Kila kukicha, tunapoteza maelfu ya wananchi kwa njia zinazoweza kuepukika. Silaha inayotuangamiza si nyingine bali ufisadi.

Usalama wetu barabarani ni duni kwa sababu ya maafisa wanaoruhusu magari mabovu kusafiri.

Nyumba tunamoishi ni kwa imani, kwani walio na majukumu ya kukagua ujenzi na kutoa vibali wanajali matumbo yao. Wataona jengo halifai kwa vile ni hatari kwa maisha, lakini kwa vile wamechotewa kitu kidogo wataacha wananchi waangamizwe.

Hakika, hii ndio hali iliyosababisha shule kujengwa kwa njia isiyofaa hadi kuporomoka wiki iliyopita na kuua watoto wanane.

Hayaishii hapo. Vyakula na vinywaji tunavyouziwa vimejaa sumu tele na vinatuua pole pole.

Nadhani tunapojigamba kuhusu jinsi tuna amani ya kutosha, shetani mpenda mauti hututazama na kucheka kwa vile hatuoni jinsi tunavyoangamizana kimya kimya kwa ulafi wetu.

Ufisadi hauhusu tu hasara inayosababishwa kwetu kwa uporaji mali ya umma jinsi wengi wetu wanaamini.

Hasara kubwa zaidi ya ufisadi ni maangamizi yanayotendwa kwetu pamoja na watoto wetu, kwani thamani ya maisha ya binadamu haiwezi kulinganishwa na kiasi chochote cha pesa za umma zinazopotelea mifukoni mwa wachache.

Tunapokataa kujitwika jukumu letu la kiraia kuhusu uongozi bora utakaopunguza ufisadi katika taifa hili, tujue ni maisha yetu tunahatarisha.

Tuna mamlaka tele kikatiba kuhusu jinsi ya kulinda maisha yetu dhidi ya viongozi walafi wasiotujali, lakini tumekataa kutambua mamlaka hayo wala kuyatumia kwa sababu wengi wetu waliamua ‘bora uhai’ bila kujua uhai wao u hatarini.

Kando na hayo, tungali tumefumbwa macho na ukabila uliokita mizizi. Maangamizi yatokanayo na ufisadi hayabagui kwa msingi wa kikabila!

You can share this post!

‘Raila, Kalonzo wafaa kustaafu’

Watahiniwa njiapanda kuhusu amri ya Magoha

adminleo