Makala

OBARA: 'Kieleweke' wamenaswa na mtego wa 'Tangatanga'

May 6th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

VIONGOZI wa kisiasa wanaoegemea upande wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga, walikuwa kwa muda mrefu wakikashifu wale wanaoonekana kuendeleza kampeni za uchaguzi wa urais wa 2022 mapema.

Tangu Uchaguzi Mkuu wa 2017 ulipokamilika na kisha baadaye Rais na Bw Odinga wakaweka mwafaka wa maelewano almaarufu kama handsheki, wafuasi wao walitofautiana na kikundi kinachoegemea upande wa Naibu Rais William Ruto, kinachompigia debe kwa urais kumrithi Rais Kenyatta.

Lakini katika siku za hivi majuzi, mambo yamebadilika kwani viongozi hawa ambao wanafahamika kama ‘Team Kieleweke’ nao pia wanafuata tabia za wale wapinzani wao walio maarufu kama ‘Team Tangatanga’.

Kwa wiki kadhaa sasa, tumejionea wanasiasa wa Kieleweke wakihudhuria mikutano ya kuchangisha pesa makanisani na hata wakiandaa mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Katika mikutano hii, wao hufanya yale yale ambayo awali walikuwa wakikashifu Tangatanga kuyahusu.

Kiongozi bora ni yule anayetenda yale anayoyasema kikamilifu, wala si anayetapatapa kwa kushikilia msimamo mmoja mchana kisha usiku yuko kwingine.

Wananchi waliokuwa wakidhani kuna viongozi wenye busara waliosimama wima kupinga siasa zinazoendelezwa makanisani na vile vile kampeni za mapema, sasa wamebaki midomo wazi kwani wale waliowadhania kuwa wangwana wamebadilika.

Hali hii ilifikia kiwango cha kuwa Sikukuu ya Leba Dei wiki iliyopita iligeuzwa kuwa ya kisiasa badala ya kusherehekea mchango wa wafanyakazi kwa uchumi wa kitaifa na kupigania masilahi yao. Zaidi ya hayo, wanasiasa wa Kieleweke walipanga kufanya mkutano wa hadhara Kakamega Jumamosi kwa madai ya kutaka kuhamasisha umma kuhusu msimamo wao wa vita dhidi ya ufisadi.

Yeyote yule anayefuatilia siasa za humu nchini kwa kina atakubaliana nami kwamba mkutano huo ulioahirishwa dakika za mwisho kama ungefanikiwa, ungekuwa tu wa kumshambulia Nibu Rais na wandani wake.

Kwa kweli, viongozi wa kundi la Kieleweke wameonyesha wazi kuwa wao ni bendera inayofuata upepo unaovumishwa na Tangatanga! B

ila shaka hii ni hali ambayo inawapa wale wa Tangatanga ari zaidi ya kuendeleza siasa zao zinazosababisha taharuki nchini kwani hakuna jinsi wataambiwa wakome, ilhali waliokuwa katika mstari wa mbele kuwakashifu nao wamejitosa ulingoni.

Tatizo linalotokea hapa ni kwamba majibizano yatazidi kutokota na kufanya iwe kama kwamba tumekaribia Uchaguzi Mkuu ilhali bado 2022 ni mbali mno.

Haya yote yatafanya wananchi wakose kuhudumiwa ipasavyo wakati huu ambapo wanakumbwa na changamoto tele za kimaisha hasa ongezeko la gharama ya bidhaa na huduma muhimu za matumizi ya kila siku.

Raia kwa sasa wanahitaji viongozi watendakazi, ambao watajiepusha na kampeni za mapema na kutekeleza wajibu waliochaguliwa kufanya.

Viongozi wanaounga mkono hatua za Rais Kenyatta na Bw Odinga za kuleta umoja na maendeleo kitaifa hawastahili kuonekana wakianguka kwenye mtego wa kampeni za 2022, na kutoa kisababu eti wanasiasa lazima wapige siasa.