Makala

OBARA: Mwaka huu kuwe na mageuzi mwafaka sekta ya elimu

January 6th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MAELFU ya wanafunzi wa shule za msingi na upili warejea shuleni leo kwa muhula wa kwanza 2020.

Ni matarajio yetu kwamba wadau wote wakuu katika sekta ya elimu wamejiandaa vya kutosha kuepusha changamoto ambazo huenda zikatatiza masomo mwaka huu.

Ingawa katika miaka ya hivi majuzi hatujashuhudia migomo ya walimu, hiyo haimaanishi walimu hawazongwi na matatizo yanayolemaza utendakazi wao.

Mwaka uliopita, kulikuwa na mvutano mkali kati ya walimu na serikali ikiwakilishwa na Tume ya Kusimamia Walimu (TSC) kuhusu utekelezaji wa mtaala mpya wa CBC.

Kuna mipango ya kupanua utekelezaji wa mtaala huo mwaka huu, kwa hivyo itahitajika kuwe na ushirikiano wa karibu kati ya TSC na walimu, hasa Chama cha Kitaifa cha Walimu (KNUT).

Kwa sasa, ni wazi kwamba mivutano tunayoona mara kwa mara kati ya mashirika hayo mawili haisaidii kwa vyovyote.

TSC inapasa kukoma kutumia vitisho dhidi ya walimu. Viongozi wa walimu pia wapasa kuwa na busara ya kukumbatia mashauriano bila kutoa masharti magumu yasiyoweza kutekelezwa.

Ni kawaida jambo lolote lile linapoanza kutekelezwa kukumbwa na changamoto.

Hakuna jinsi changamoto hizo zitatatuliwa kama wadau wakuu watashiriki kwenye vita vya ubabe nyakati zote.

Waathiriwa ni wanafunzi ambao watapakuliwa mtaala duni kwa vile wahusika walikataa kushirikiana kung’oa visiki vilivyopo.

Isitoshe, watoto wanarudi shuleni baada ya likizo ndefu ya takriban miezi miwili.

Wakati huo wote, kuna wengi wao walipewa uhuru mwingi nyumbani ambao huenda ukaathiri nidhamu yao wanaporudi shuleni.

Mwaka uliopita, ripoti kuhusu utovu wa nidhamu hazikutanda sana kama ilivyokuwa katika miaka ya awali. Hii ni pamoja na visa vya shule kuchomwa, ulevi wa watoto miongoni mwa maovu mengine ya kijamii.

Kama ilivyo ada, enzi hizi wazazi wengi huwa hawatengi muda wa kutosha kufahamu yale ambayo watoto wao hufanya wakati wa likizo.

Kwa msingi huu, hakutakosekana watoto ambao wanarudi shuleni wakiwa na tabia mbovu walioiga mitaani tofauti na walivyokuwa mwaka uliopita.

Nina imani walimu wengi katika shule zetu wana ujuzi kuliko idadi kubwa ya wazazi nchini kutambua watoto wanapoanza kupotoka kimaadili.

Wito ni kwamba, walimu wajitolee bila kuchoka kuzima tabia hizo kabla zienee kwa wanafunzi wengine na kuzua balaa shuleni.

Vile vile, tusisahau jinsi visa vya watoto kujitoa uhai vinavyozidi kuongezeka. Hili ni suala linalohitaji kuchunguzwa kwa makini ili visa aina hiyo vizuiwe mwaka 2020.