Makala

OBARA: Ni wajibu wa kila mmoja wetu kufichua matapeli

May 19th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

INATIA moyo mno kuona jinsi watu wanaoshukiwa kujitajirisha kwa njia za kiharamu wanavyozidi kunaswa na maafisa wetu wa usalama.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) inastahili pongezi kwa juhudi zake za kutuondolea matapeli na wezi wa mali ya umma wanaoishi miongoni mwetu.

Vita vilivyoanza kwa kunasa washukiwa wa ufisadi, vikaenda kwa wafanyabiashara wanaoingiza bidhaa haramu nchini, sasa vimetamba na kuelekea kwa walaghai ambao kazi yao ni kutengeneza pesa haramu za kigeni na dhahabu feki.

Kwa muda mrefu, vijana wamekuwa wakitamani sana kuwa kama viongozi na wafanyabiashara matajiri wanaowaona katika jamii.

Ni kawaida vijana wengi kuwa na hamu ya kupata utajiri kwa haraka ili waishi maisha ya starehe itakayowawezesha kusafiri kule wanakotaka, kumiliki nyumba kubwa kubwa na kuendesha magari ya kifahari.

Mitandao ya kijamii haijasaidia kuondolea vijana hamu ya kupata utajiri kwa haraka kwani kila unapoingia kwenye mitandao hii, unachopata ni picha za mabwanyenye hao wakijigamba jinsi wanavyoponda raha.

Kwa kukamata wezi na matapeli na kuzuilia mali zao, DCI inasaidia kuonyesha jamii kwamba hakuna faida kwa yeyote kujitajirisha kwa mali haramu.

Juhudi hizi hazifai kukomea katika kukamata washukiwa, bali tungependa kuona wakiadhibiwa. Ni kupitia adhabu kali pekee ambapo tutaamini kuhusu umuhimu wa kutafuta riziki kwa njia za haki.

Tunakumbuka katika miaka iliyopita kuna watu waliowahi kukamatwa kwa makosa sawa na haya tunayoona hivi sasa lakini kesi zao zikatokomea kwa njia zisizoeleweka.

Kuna wengine wetu wanaohofia kwamba huenda pia wale mamia ya washukiwa waliokamatwa kufikia sasa huenda wasiadhibiwe. Shaka hii imekita mizizi hasa ikizingatiwa jinsi kuna baadhi ya maafisa wa upelelezi wanaoaminika hushirikiana na washukiwa kuvuruga kesi zao.

Vile vile, hatuwezi kusahau mahakamani pia kuna mahakimu, majaji na hata maafisa wengine wa korti wanaoweza kutumia mamlaka yao kuvuruga kesi kwa sababu ya kupokezwa mabunda ya noti.

Tumepotosha vijana kwa muda mrefu kama jamii na kufanya wengi wao waishie kuwa wakora kwa vile tunavyosifu mabwenyenye ambao hatujui historia yoyote kuhusu jinsi walivyopata mali zao.

Hawa ndio watu tunaochagua kuwa viongozi wetu wa kisiasa. Makanisani, wengi wao ndio wazee wa kanisa kwa sababu ya donge nono wanalotoa kama zaka na sadaka. Shuleni, tunataka wasimamie makundi ya wazazi kwa sababu ya ushawishi walionao.

Jamii ina nafasi bora hivi sasa ya kuhimiza vijana kujiepusha na njia za mkato za kujitafutia mali. Ni njia hizi za mkato ambazo zimeingiza wengi katika aina nyingine hatari za uhalifu ikiwemo ugaidi na ulanguzi wa dawa za kulevya.

Sasa itakuwa muhimu kwa kila mmoja wetu katika jamii kutekeleza wajibu wake kwa njia yoyote inayoweza kusaidia kutuondolea matapeli, walaghai na wezi wa umma wanaoishi miongoni mwetu.

Hii haitakuwa kazi rahisi ndiposa inahitaji ushirikiano wa asasi zote husika, ikiwemo idara ya mashtaka ya umma mbali na polisi, mahakama na jamii kwa jumla.