Makala

OBARA: Tutatue vikwazo vya ajira badala ya kuimbaimba 'Vijana Wajiajiri'

August 6th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MAHALI tulipofika sasa, wimbo huu wa ‘Vijana Wajiajiri’ wasinya!

Kila mara mdahalo unapoibuka kuhusu janga la ukosefu wa ajira kwa vijana Kenya, utasikia sauti nzito kutoka pembe tofauti zikiwika: “Vijana wajiajiri.”

Wakati mwingi, sauti hizo huwa zinatoka kwa watu waliokalia viti vya kifahari afisini walimoajiriwa. Wengine wao ni watumishi wa umma, kumaanisha ni waajiriwa wa raia wale wale ambao wanashurutisha kujiajiri.

Sina pingamizi kuhusu umuhimu wa ujasiriamali katika enzi hizi ikizingatiwa kwamba hali ya maisha imebadilika na hakuwezi kuwepo nafasi za kutosha kuajiri afisini kila kijana anayekamilisha elimu ya juu.

Lakini jinsi mdahalo kuhusu ukosefu wa ajira unavyoendeshwa, ni kama kwamba tunalaumu vijana kwa uzembe na upumbavu unaowakosesha uwezo wa kujiajiri wenyewe.

Changamoto zinazokumba vijana kikazi zimesababishwa na masuala tofauti ambayo yanastahili kuzingatiwa kwa uzito zaidi kuliko kujaribu kulazimisha kila kijana kuwa mjasiriamali hata kama hana uwezo huo.

Ujasiriamali stadi hauhitaji tu mafunzo ya darasani wala ya kiufundi au hela za kuwekeza. Kuna ujuzi fulani ambao mtu huzaliwa nao ndipo afanikiwe, na ukitaka kujua ukweli huu, tazama tu wajasiriamali waliobobea kimataifa na ukague wasifu wao.

Mwaka uliopita, Benki Kuu ya Kenya ilifichua kwamba zaidi ya asilimia 61 ya biashara ndogo ndogo huwa hazikamilishi miaka miwili kabla kufungwa. Waimbaji wa ‘Vijana Wajiajiri’ wameamua kufumbia macho takwimu hizi!

Mfumo wetu wa elimu umebainika kuwa ovyo na unaohitaji mabadiliko. Itachukua muda kabla tuone mafanikio ya juhudi zinazoendelezwa sasa kubadilisha mfumo wa elimu, hivyo basi hebu tuangalie masuala mengine yatakayoboresha hali kwa dharura.

Ufisadi ni mojawapo ya vikwazo vinavyozuia vijana kujiendeleza kimaisha hata wakijitosa katika biashara. Kisheria, asilimia 30 za zabuni serikalini zinafaa ziende kwa vijana. Lakini kufikia sasa, tunachoshuhudia ni zabuni kutolewa kwa njia za ufisadi na kujuana kisha viongozi wao hao wanaohusika ndio huja kutuambia vijana wajiajiri!

Vilevile, mandhari ya kufanya biashara katika nchi hii ni duni mno. Mashirika mengi makubwa ya kimataifa yalishindwa kustahimili mandhari magumu ya kuendesha biashara Kenya, sembuse vijana ambao ndio wanajaribu bahati yao kwa biashara ndogo ndogo!

Zaidi ya hayo, sheria za uhamiaji zinastahili kutekelezwa kikamilifu ili kuzuia raia wa kigeni kunyakua kazi zinazoweza kufanywa na Wakenya.