MakalaSiasa

OBARA: Twahitaji muujiza wa pili ili mwafaka ufanikiwe

August 6th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

Baada ya kusubiri kwa miezi mitano, hatimaye mojawapo ya malengo makuu ya muafaka baina ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga imeanza kutekelezwa.

Kamati maalum iliyobuniwa na wawili hao tayari imetoa wito kwa wananchi kuwasilisha maoni yao kuhusu jinsi ya kupambana na ufisadi.

Ingawa hii ni hatua bora katika kuendeleza mbele malengo ya muafaka huo, kuna wasiwasi kwamba kamati hii huenda ikaishia tu kuwa kama zingine nyingi ambazo zimewahi kuwepo katika miaka iliyopita.

Kenya imekuwa maarufu kwa uundaji wa kamati na majopokazi chungu nzima kila mara tunapokumbwa na changamoto mbalimbali lakini kinachosikitisha ni kuwa, ripoti zinazotolea huwa hazitekelezwi.

Hii ni licha ya kuwa kamati hizo hutumia rasilimali za umma kuendeleza shughuli zao ikiwemo kutumia fedha zinazotoka katika kapu linalofadhiliwa na mlipaushuru.

Hakika, masuala mengi ambayo Bw Odinga na Rais Kenyatta walitaja kuwa changamoto wanazolenga kutatua yamewahi kuchunguzwa.

Mfano ni suala kuhusu utendaji wa haki sawa kwa kila mwananchi bila kujali kabila, tabaka wala misimamo ya kisiasa.

Hili ni jambo ambalo lilichunguzwa kwa kina mno na Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) ambayo ilitumia muda na rasilimali tele za umma kuzunguka nchini kote kushauriana na wananchi.

Tume hiyo ilikusanya malalamishi na maoni ya Wakenya hasa kutoka jamii zilizokuwa zimekandamizwa kihaki katika tawala zilizopita.

Utoaji wa ripoti ya tume hiyo ulikumbwa na utata kwa kuwa ilitoa mapendekezo yaliyoshutumu watu mashuhuri nchini kwa kudhulumu haki za raia wa kawaida.

Hatimaye ripoti ilipotolewa, kulikuwa na minong’ono kwamba haikuwa ripoti halisi bali ilifanyiwa ukarabati. Hata hivyo, ripoti hiyo iliyotolewa haijatekelezwa kufikia sasa.

Masuala mengine mengi ambayo yamewahi kuchunguzwa na kamati tofauti ni kuhusu mauaji ya kikatili ya raia na pia ya viongozi mashuhuri, mbali na suala sugu la unyakuzi wa ardhi.

Kwa mtazamo wangu, kamati iliyobuniwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga haingepoteza muda mwingi ila kurejelea ripoti hizo zote na kupendekeza kinachofaa kutekelezwa kutoka kwazo.

Kuna hatari ya kamati hii kutumia muda na rasilimali tele kisha mwishowe ije na mapendekezo yale yale ambayo yamewahi kuwasilishwa kwetu.

Wakifanya hivyo, natumai malaika aliyetenda muujiza wa kuwapatanisha viongozi hao wawili kisiasa atakuwa bado anatembeatembea humu nchini ili atende muujiza mwingine wa kufanya ripoti itakayotolewa itekelezwe kikamilifu.

Bila hilo, tujiandae tu kurudi uchaguzini 2022 tukiwa tungali tumebeba mzigo huu mzito wa matatizo ya ufisadi, ukiukaji wa haki za kibinadamu, dhuluma za kikabila miongoni mwa mengine.

Tuna nafasi bora ya kupata mabadiliko ambayo yatasaidia kuboresha maisha ya wananchi wa kawaida lakini hilo litawezekana tu kama viongozi wetu watajitolea kuweka kando maslahi yao ya kibinafsi kwa muda.