Makala

OBARA: Uganda itavuna pakubwa huku Wakenya wakiumia

April 1st, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

ZIARA ya Rais Yoweri Museveni wa Uganda humu nchini wiki iliyopita iliacha wananchi wengi na viongozi kadha vinywa wazi kwa mshangao.

Katika ziara hiyo ambayo serikali ilidai ilinuia kuimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili, ukweli mchungu ni kwamba, Uganda inaonekana kunufaika zaidi.

Kwanza, Kenya imekubali kufungua milango yake kwa msururu wa bidhaa ambazo zitakuwa zinaingizwa kutoka Uganda. Bidhaa hizo ni kama vile sukari, kuku na maziwa.

Haya yanajiri wakati wakulima wetu wanateseka sana kwa sababu ya jinsi wafanyabiashara wanavyoagiza bidhaa za kilimo kwa bei ya chini kutoka nchi za nje.

Bidhaa kama vile mayai, mahindi na vitunguu hufurika masoko yetu kutoka nchi tofauti ikiwemo Uganda na kuuzwa kwa bei ya juu kuliko zile zinazozalishwa nchini.

Matokeo yake ni kwamba, wakulima wa Kenya hulazimika kupunguza bei za bidhaa zao na ingawa hili hufurahisha wateja, wakulima hupata hasara kubwa kwa hali inayoathiri uchumi wa taifa mbali na uwezo wao wenyewe kujikimu kimaisha.

Nafahamu kwamba serikali yetu, ikiongozwa na Rais Uhuru Kenyatta inataka kumvutia Rais Museveni ili abadili msimamo wake wa awali ambao ulitishia kuathiri uchumi wetu.

Ninakumbuka vyema jinsi miaka michache iliyopita, Rais Museveni alivyobadili ghafla msimamo wa awali wa nchi yake kushirikiana na Kenya kustawisha sekta ya uchimbaji na usafirishaji mafuta na badala yake, akaamua kushirikiana na Tanzania.

Vile vile, kuliibuka ripoti baadaye kuhusu jinsi Uganda ilivyokuwa na tashwishi kuhusu reli ya kisasa maarufu kama SGR ilhali mpango wa awali ulikuwa mataifa haya mawili yaungane ili mizigo iwe ikisafirishwa kati ya bandari ya Kenya na taifa la Uganda moja kwa moja kupitia kwa reli.

Kwa muda huo wote, Rais Museveni alionekana kulenga kushirikiana na Rwanda na Tanzania badala ya Kenya. Kwa sasa, yeyote anayefuatilia habari za bara hili la Afrika, hasa ukanda wa Afrika Mashariki, anafahamu uhusiano kati ya Uganda na Rwanda unazidi kudorora.

Bila shaka, Rais Kenyatta ameuchukulia wakati huu kuwa mwafaka zaidi kumshawishi mwenzake wa Uganda kulegeza misimamo yake ya awali ili warejelee mipango ya awali.

Sikatai bandari yetu ya Mombasa ni rasilimali muhimu inayohitaji kuhakikishiwa inapata faida tele mara kwa mara. Hakika, reli yetu mpya pia imetugharimu hela nyingi na serikali inahitajika kutafuta kila namna ya kupata faida kutoka kwa muundomsingi huo.

Kwa msingi huu, ni muhimu kustawisha uhusiano wetu na majirani hasa Uganda ambalo ni taifa linalolazimika kutegemea majirani wake kwa uagizaji au uuzaji bidhaa kupitia baharini.

Hata hivyo, hakutakuwa na manufaa yoyote kama tutakuza sehemu moja ya uchumi na kuangamiza nyingine, hasa sekta ya kilimo, kwa kuagiza bidhaa za nje ambazo tunaweza kujizalishia wenyewe.

Serikali itilie maanani zaidi uwekezaji katika mbinu ambazo zitasaidia wawekezaji katika kila sekta kuzalisha bidhaa kwa bei nafuu ili kuwalinda kutokana na bidhaa za bei ya chini zinazotoka ugenini.