Makala

OBARA: Ununuzi wa vitabu shuleni usiachiwe walimu wakuu

March 24th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MATUKIO yenye umuhimu mkubwa katika sekta ya elimu yalishuhudiwa wiki iliyopita.

Kwa bahati mbaya, hayakufanikiwa kupewa uzito inavyostahili kwenye midahalo yetu ya kila siku, hasa kwa sababu wengi wetu kwa sasa wameelekeza macho yao katika njaa inayokeketa wenzetu katika sehemu mbalimbali za nchi.

Masuala yenyewe yaligusia misimamo tofauti kati ya serikali na walimu kuhusu utekelezaji wa mtaala mpya, uhamisho wa walimu na usambazaji vitabu kwa shule za umma.

Kilichonivutia zaidi ni maoni ya mmoja wa maafisa wa vyama vya walimu kuhusu usambazaji vitabu shuleni.

Wawakilishi wa vyama vya walimu wakuu wa shule za msingi na upili walipokuwa mbele ya kamati ya bunge inayosimamia elimu, ilibainika wangependa jukumu hilo lirudishwe mikononi mwao.

Wakati Dkt Fred Matiang’i alipokuwa Waziri wa Elimu, Serikali iliamua kutwaa jukumu hilo kutoka kwa walimu wakuu.

Bila shaka, kulikuwa na sababu mwafaka zilizochochea uamuzi huo, kuu kati yao ikiwa ni ufisadi uliokithiri miongoni mwa baadhi ya walimu wakuu. Ilidaiwa wengine wao walikuwa wakishirikiana na wachapishaji vitabu au wauzaji vitabu kupunja walipaushuru na wazazi.

Kwa msingi huu, inashangaza tunaposikia walimu wakuu wakipendekeza warudishiwe jukumu hilo.

Kile ambacho ningetarajia kusikia kutoka kwao kama Serikali inakumbwa na changamoto, ni wito wa ushirikiano kati ya wadau ili shughuli nzima ifanywe kwa njia itakayonufaisha mahitaji ya wadau wote, hasa wanafunzi na walimu.

Haishangazi kwamba Serikali inapitia matatizo kufanikisha usambazaji huo wa vitabu shuleni kwa njia ambayo ingetarajiwa.

Changamoto za kila aina huwepo wakati wowote mfumo wa utendakazi unapobadilika, hasa kwa asasi za serikali.

Malalamishi kwamba baadhi ya shule hupokea vitabu vichache kuliko inavyotakikana, na vingine kupokea vingi kupitia kiasi ni jambo ambalo hata halingefika bungeni.

Walimu wakuu wakishirikiana na maafisa wa serikali wanaosimamia elimu katika maeneo yao, nina hakika vizingiti kama hivi vinaweza kutatuliwa kwa urahisi.

Hatua ya walimu wakuu kusisitiza kwamba wasimamie usambazaji vitabu kwa shule zao lilinikunbusha tu kuhusu jinsi wachanganuzi wa masuala ya uongozi na kisiasa wanavyosema mara kwa mara kwamba kila asasi ya serikali na viongozi wana wakati wao wa ‘kula’.

Jukumu hilo lilitwaliwa kutoka kwa walimu kufuatia madai ya ufisadi na sasa kuna wanaoamini ufisadi uliokuwepo ungali upo ila walaji ndio wamebadilika.

Kama ni kweli tumeshindwa kuzuia ulaji huo haramu, angalau tuhakikishe watoto wanapata haki yao badala ya kutaka ‘sinia’ izungushwe kutoka meza hii hadi ile kwa zamu.

Hii itawezekana tu ikiwa mivutano itakomeshwa, kuwe na ushirikiano kwa wadau wote.

Natumai waziri wa elimu mteule, Prof George Magoha atachukulia suala hili kwa uzito.

[email protected]