Makala

OBARA: Vijana waliofuzu vyuoni watafute njia za kujikimu

December 24th, 2018 2 min read

Na VALENTINE OBARA

KWA wiki kadhaa mwezi huu hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, mamia ya maelfu ya wanafunzi walifuzu kwa shahada mbalimbali kutoka vyuo vikuu nchini na taasisi nyinginezo za mafunzo ya elimu ya juu.

Kama ilivyo kawaida, mahafali yalifuatwa na sherehe za aina yake kwa idadi hiyo kubwa ya wanafunzi kwani wengi wao sasa wanatarajia kuingia sehemu mpya maishani mwao.

Swali ambalo wakati mwingi huibuka wakati wa hafla hizi kutoka kwa jamaa na marafiki huwa ni kuhusu kile ambacho mwanafunzi anayefuzu anatarajia baada ya hapo.

Kuna walio na matarajio ya kupata ajira, wanaotazamia kuanzisha au kuinua biashara zao ndogo kwa kutumia ujuzi waliopata vyuoni na vile vile, kuna wanaotazamia kupandishwa vyeo katika maeneo wanamofanya kazi.

Kati ya hawa wote, wanaokumbwa na shinikizo kubwa la kubadilisha maisha yao baada ya kufuzu kutoka vyuoni ni wale vijana wadogo walio na matumaini ya kuajiriwa kwa mara ya kwanza.

Hawa ni vijana ambao wengi wao wangali wanaishi na wazazi au jamaa zao na baada ya kukamilisha elimu ya juu, wanahitajika waanze kujitegemea na hata kutegemewa kusaidia wadogo wao au wazazi na jamaa wengine kiriziki.

Kinachosikitisha ni kwamba idadi ndogo mno kati yao ndio watafanikiwa kupata ajira kwa haraka kwani kama tujuavyo, Kenya ingali inakumbwa na uhaba wa nafasi za ajira na hali hii inazidi kuwa mbaya kadri na jinsi miaka inavyosonga.

Inahitajika vijana hawa wahimizwe wachukue muda kutambua talanta walizo nazo kujitafutia riziki hata wanapoendelea kutafuta kazi za ofisini wanazozitamani.

Wito ni kwa wasomi kuacha kuomba serikali kuwasaidia bali wao wenyewe watambue jinsi wanavyoweza kujisaidia kwa njia itakayoleta manufaa kwa taifa zima.

Vile vile, katika enzi hizi, kuna changamoto tele katika jamii zinazohitaji ubunifu kutatuliwa na vijana hawa waliotoka vyuoni wana uwezo wa kubuni mbinu mbadala za kutatua changamoto zilizopo kwa njia itakayowaletea riziki.

Hiki ni kizazi kilicho na ujuzi mkubwa wa kutumia teknolojia za kisasa na kama watapewa rasilimali wanazohitaji, vijana wanaweza kusaidia sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya na elimu kuweka mikakati ya kisasa ya utendakazi na utoaji huduma kwa njia bora zaidi.

Kile ambacho waliofuzu kutoka vyuoni wanahitaji kujiepusha nayo ni kukaa mitaani au vijijini bila kufanya kazi yoyote kwani hali hii ndiyo huwaletea wengi wao mawazo ya kutenda maovu.

Hapo ndipo utakuta wakijiunga na makundi ya kihalifu huku wengine wakitumia kisomo chao kutekeleza uhalifu wa kisasa kama vile wizi wa kidijitali mitandaoni.

Ni muhimu ieleweke kwamba manufaa ya uhalifu ni ya muda mfupi, bali athari yake ni ya kudumu kwa mtu binafsi, familia yake na hata jamii kwa jumla.