Michezo

Obiri afuta machozi baada ya kujishindia dhahabu na rekodi

October 7th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HELLEN Obiri alifuta machozi ya kukosa medali kwenye mbio za mita 10,000 kwa kuhifadhi taji lake la mbio za mita 5,000 kwenye Riadha za Dunia jijini Doha, Qatar.

Obiri, ambaye sasa anajivunia medali tano katika mbio za mita 5,000 baada ya kuzoa dhahabu kwenye Riadha za Dunia mwaka 2017 na 2019, fedha kwenye Olimpiki (2016), Jumuiya ya Madola (2018) na Bara Afrika (2018), alimaliza mbio za mita 10,000 katika nafasi ya tano.

Mnamo Jumamosi, Obiri aliamua kutumia mbinu tofauti katika mizunguko 12 na nusu baada ya zile za kubadilishana uongozi kufeli katika mbio za mizunguko 25.

Alikwamilia uongozi mzunguko wa kwanza ulipokamilika na kuhifadhi taji kwa muda wa dakika 14:26.72, ambao ni rekodi mpya ya mbio za mita 5,000 kwenye Riadha za Dunia.

Alifuta rekodi ya dakika 14:26.83 ya Muethiopia Almaz Ayana aliyoweka mwaka 2015 jijini Beijing.

Obiri alifuatwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Margaret Chelimo (14:27.49), Mjerumani Konstanze Klosterhalfen (14:28.43), Muethiopia Tsehay Gemechu (14:29.60) na Mkenya mwingine Lillian Kasait (14:36.05).

 

Mkenya Hellen Obiri akisherehekea kwa kupeperusha bendera ya taifa baada ya kushinda mbio za mita 5,000 kwa upande wa akina dada katika Riadha za Dunia mnamo Oktoba 5, 2019, uwanjani Khalifa jijini Doha. Picha/ AFP

Baada ya kunyakua taji lake la pili mfululizo kwenye Riadha za Dunia, Obiri alifichua bado azma yake ni kuvuna medali katika mbio za mita 10,000.

“Tuna wakimbiaji wazuri nchini Kenya. Nilitia bidii zaidi kuthibitisha tuna uwezo wa kushinda. Haikuwa rahisi kupata rekodi ya mashindano haya bila wawekaji kasi. Hata hivyo, mashabiki walinipa nguvu na nikasalia makini.

“Msimu ulikuwa mrefu kutoka zile za kufungua msimu za mbio za nyika, Riadha za Diamond League, halafu mashindano haya; nadhani nitachukua likizo ya mwezi mmoja. Pengine nitajaribu tena mbio za mita 10,000 kwenye Olimpiki.

Chelimo alifurahia kuvuna medali yake ya kwanza katika Riadha za Dunia. “Miaka miwili iliyopita jijini London, nilimaliza katika nafasi ya tano. Leo (Jumamosi) nimepata nishani ya fedha. Nafurahia sana mafanikio haya. Nafurahia kupata medali hii jijini Doha kwa sababu nilipokuwa hapa kwa mbio za Diamond League sikuhisi vyema, sikuwa katika hali nzuri. Nalenga sasa kuwa katika Olimpiki mwaka ujao. Natumai nitapata medali pia.