Michezo

Obiri alenga juu zaidi huku Kipyegon na Rotich wakiwika pia Doha Diamond League

September 26th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA mara tatu wa dunia, Hellen Obiri, aliandikisha muda bora zaidi duniani katika kampeni za Wanda Diamond League kwa mara ya pili mwaka 2020.

Malkia huyo wa mbio za mita 5,000 duniani alikamilisha mbio za mita 3,000 katika Doha Diamond League jijini Qatar kwa dakika 8:22.54 mnamo Ijumaa usiku na kukaribia dakika 8:20.68 ambao ndio muda bora zaidi anaojivunia katika fani hiyo.

Obiri aliwahi kutamalaki duru ya kwanza ya Diamond League msimu huu alipokamilisha mbio za mita 5,000 kwa muda bora wa dunia (dakika 14:22.12) jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14.

Alisalia katika nafasi ya pili kwa muda mrefu jijini Doha huku akisoma mgongo wa Mkenya mwenzake Winny Chebet aliyefikia hatua ya mita 1,000 kwa muda bora wa dakika 2:48.46 kabla ya kupitwa na Obiri.

Zikisalia mita 500 pekee, Beatrice Chepkoech alichukua usukani kutoka kwa Obiri ila bingwa huyo wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji hakuongoza kwa kipindi kirefu kabla ya kuzidiwa maarifa na Obiri katika mita 300 za mwisho.

Mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 10,000 duniani, Agnes Jebet aliambulia nafasi ya pili kwa muda wa dakika 8:22.92 mbele ya Chepkoech aliyeridhika na nafasi ya tatu (8:22.93).

Wakenya wengine waliowika katika mbio hizo ni mshindi wa medali ya fedha katika mbio za mita 5,000 duniani, Margaret Chelimo (8:24.76) na mshindi wa fedha katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye Olimpiki, Hyvin Kiyeng (8:25.13).

“Huu haujakuwa msimu bora kwa kila mmoja. Hata hivyo, furaha ni kwamba kipindi hiki kigumu kinaelekea kutamatika,” akatanguliza Obiri.

“Sasa naelekeza macho kwa kampeni za mwaka ujao ambapo natazamia kuendeleza ubabe wangu kwenye Olimpiki za Tokyo. Narejea jijini Nairobi nikiwa mwingi wa fahari,” akaongeza.

Zikisalia mita 200 pekee, Faith Chepng’etich Kipyegon alifyatuka na kukamilisha kivumbi cha mita 800 kwa muda wa kasi zaidi msimu huu. Bingwa huyo wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 alisajili muda wa dakika 1:57.68.

Kipyegon, 26, alitamalaki mbio za mita 1,000 (dakika 2:29.32) jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14 kabla ya kuandikisha muda wa dakika 2:29.92 jijini Brussels, Ubelgiji mnamo Septemba 4. Katika duru hizo, alikuwa pua na mdomo kuvunja rekodi ya dunia ya dakika 2:28.98 iliyowekwa na Mrusi Svetlana Masterkova katika mbio za mita 1,000 mnamo 1996.

Alirejea kushiriki mbio za mita 1,500 jijini Ostrava kwenye Riadha za Dunia za Continental Gold Tour zilizoandaliwa katika uwanja wa Mestky, Jamhuri ya Czech mnamo Septemba 8. Alisajili muda wa dakika 3:59.05 na kufuta rekodi ya dakika 4:00.96 iliyowekwa na Mwethiopia Gudaf Tsegay mnamo 2017.

“Ni tija kubwa kuibuka mshindi katika mbio za mita 800 ambazo nimezishiriki kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu. Sikutarajia kabisa kushinda wala kuweka rekodi mpya,” akasema Kipyegon aliyembwaga Mhispania Esther Guerrero (1:59.22).

Emily Cherotich aliyekamilisha mzunguko wa kwanza kwa sekunde 57.72 katika mbio hizo aliambulia nafasi ya nne nyuma ya Mwingereza Adelle Tracey (1:59.87).

Licha ya ushindani mkali kutoka kwa Wycliffe Kinyamal, Erik Sowinski wa Amerika na Mwingereza Giles Elliot, Ferguson Rotich aliibuka mshindi wa mbio za mita 800 kwa upande wa wanaume jijini Doha. Aliandikisha muda wa dakika 1:44.17 na kumpiku bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot.

Rotich, alijitwalia nishani ya shaba katika mbio za mita 800 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar mnamo 2019. Alitupwa hadi nafasi ya nane katika duru ya Diamond League jijini Monaco (1:45.48) kabla ya kujinyanyua na kuambulia nafasi ya nne (1:45.11) jijini Stockholm, Uswidi mnamo Agosti 23, 2020.