Michezo

Obiri ashindia Kenya shaba ya marathon, Kenya ikikamilisha Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE August 11th, 2024 1 min read

KENYA imefunga makala ya 33 ya Michezo ya Olimpiki kwa nishani ya shaba kupitia kwa bingwa wa Boston Marathon, Hellen Obiri mjini Paris nchini Ufaransa, Jumapili, Agosti 11, 2024.

Mkazi wa Amerika, Obiri, 34, amekamilisha mbio hizo za kilomita 42 kwa saa 2:23:10, nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan (2:22:55) na mshikilizi wa rekodi ya dunia Tigst Assefa kutoka Ethiopia (2:22:58) walionyakua dhahabu na fedha, mtawalia.

Zikisalia kilomita sita, vita vilikuwa kati ya Sharon Lokedi (Kenya), Amane Beriso na Assefa (Ethiopia), Obiri na Hassan. Mambo hayakuwa tofauti zikisalia kilomita 3 hadi karibu kilomita ya mwisho wakati Assefa alichomoka, lakini akafuatwa unyo kwa unyo na Hassan aliyemzima katika mita 200.

Wakenya Sharon Lokedi na Peres Jepchirchir (aliyekuwa akitetea taji), waliridhika na nafasi ya nne na 15 kwa 2:23:14 na 2:26:51, mtawalia.

Joyce Chepchumba alishinda medali ya kwanza kabisa ya marathon kwenye Olimpiki alipopata shaba mwaka 2000 mjini Sydney, Australia.

Kutoka hapo, Kenya ilipata fedha kupitia kwa Catherine Ndereba (2004 na 2008) na Priscah Jeptoo (2012) na kuzoa dhahabu kupitia kwa Jemima Sumgong (2016) na Peres Jepchirchir (2020). Brigid Kosgei alinyakua fedha mwaka 2020.

Matokeo ya marathon ya wanawake Jumapili yanamaanisha kuwa Kenya imeachilia ubingwa ambao ilikuwa imeshinda mara mbili mfululizo.

Mbali na kuibuka bingwa mpya wa Olimpiki, Hassan pia aliweka rekodi mpya ya Olimpiki ya marathon ya wanawake baada ya kufuta ile ya 2:23:07 Muethiopia Tiki Gelana aliweka mwaka 2012.