Obiri atawala 10,000m Kasarani, zamu ya Omanyala ni leo Jumamosi

Obiri atawala 10,000m Kasarani, zamu ya Omanyala ni leo Jumamosi

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Hellen Obiri, Winny Chebet na Mary Moraa ni baadhi ya watimkaji waliong’ara katika siku ya kwanza ya mashindano ya kuchagua timu ya taifa ya Kenya itakayoshiriki Riadha za Dunia na michezo ya Jumuiya ya Madola mwezi ujao wa Julai.

Bingwa wa dunia mita 5,000 Obiri alikamilisha mbio za kuzunguka uwanja mara 25 kwa dakika 31:49.88.

Malkia wa zamani Afrika mita 5,000 Sheila Chepkirui (31:50.13) na mshindi wa nishani ya shaba ya dunia mita 5,000 Margaret Chelimo (31:50.22) walifunga mduara wa tatu-bora mtawalia. Obiri aliwatoka wapinzani hao wake wa karibu zikisalia mita 200.

Malkia wa Afrika mita 1,500 Winny Chebet alitawala kitengo hicho alipokata utepe kwa dakika 4:11 21. Mshindi wa nishani ya fedha ya Afrika riadha za Under-20 Edna Jebitok na Purity Chepngetich walimfuata Chebet mtawalia.

Watimkaji wa mbio fupi Mike Mokamba na Maximilla Imali walinyakua mataji ya mita 200. Mokamba alitumia sekunde 20.70 akifuatiwa kwa karibu na Dan Kiviasi (20.8) wote wakiingia Jumuiya ya Madola. Imali aliweka rekodi mpya ya kitaifa alipomaliza kwa sekunde 23.37. Alivunja rekodi yake ya 23.6 aliyoweka Aprili. Millicent Ndoro alifuata kwa 23.5. Imali na Ndoro walijikatia tiketi ya Jumuiya ya Madola.

Nicholas Kimeli (dakika 13:28.76), Jacob Krop (13:29.30) na Cornelius Kemboi (13:29.90) walifagia nafasi tatu za kwanza mita 5,000 za wanaume.

Mshindi wa nishani ya fedha mita 800 shindano la Kip Keino Classic Mary Moraa aliimarisha muda wake bora kutoka 1:58.93 hadi dakika 1:57.45 aliopata kwenye duru ya Diamond League mjini Rabat, Morocco mnamo Juni 5. Moraa alifuatwa kwa karibu na malkia wa mita 1,500 Faith Kipyegon (1:58.18) na bingwa wa Afrika Jarinter Mawia (2:00.36).

Naye mfalme wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi riadha za dunia za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 Amos Serem aliduwaza wazoefu. Alichomoka katika mzunguko wa mwisho na kushinda kwa dakika 8:17.03. Aliwaonyesha kivumbi mshindi wa nishani ya shaba ya Jumuiya ya Madola Abraham Kibiwott na bingwa wa dunia Conselsus Kipruto waliridhika na nafasi mbili waliofuatana katika usanjari huo.

Mashindano hayo yanaingia siku ya pili na mwisho leo Jumamosi, Juni 25 ambapo mmoja wa vivutio ni mshikilizi wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yaonya wasafiri kuhusu magaidi

Uhuru ajipanga asitikiswe na Karua Mlimani

T L