Obiri atawala mbio za kilomita 21 za Great North Run

Obiri atawala mbio za kilomita 21 za Great North Run

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Hellen Obiri ameendeleza utawala wa akina dada kutoka Kenya wa kutwaa mataji ya mbio za kilomita 21 za Great North Run hadi miaka minane leo Jumapili.

Obiri amenyakua taji kwa saa 1:07:42 katika mbio hizo zilizofanyika katika miji ya Newcastle na Gateshead nchini Uingereza.

Alifuatwa sekunde 0.06 baadaye na Muingereza Eilish McColgan (1:07:48) naye Charlotte Purdue, pia kutoka Uingereza, akafunga mduara wa tatu-bora (1:08:49).

Obiri alishiriki nusu-marathon yake ya kwanza kabisa mnamo Aprili 4 mwaka huu – N Kolay Istanbul Half Marathon nchini Uturuki – ambayo alimaliza katika nafasi ya tatu kwa saa moja dakika nne na sekunde 51.

Mshikilizi huyo wa rekodi ya kitaifa ya mbio za mita 5,000 amefuata nyayo za watangulizi wake kutoka Kenya, Mary Keitany (2014, 2015 na 2017), Vivian Cheruiyot (2016 na 2018), Priscah Jeptoo (2013) na Brigid Kosgei (2019).

Uingereza nayo ilinyakua taji lake la saba mfululizo la wanaume kupitia kwa Marc Scott (1:01:22).

Mwingereza Mo Farah alikuwa ameshinda mataji sita yaliyopita. Scott alifuatiwa kwa karibu na Mkenya Edward Cheserek anayeishi nchini Amerika (1:01:31) na Mwamerika Galen Rupp (1:01:52) mtawalia.

Wakenya Kosgei na Martin Mathathi wanashikilia rekodi ya Great North Run ya saa 1:04:28 na dakika 58:56, mtawalia.

You can share this post!

Fidu aahidi makubwa kwa mashabiki wa Changamwe Ladies

KAMAU: Mapinduzi yanatoa dalili Afrika imeshindwa kujitawala