Michezo

Obiri avunja rekodi kwenye mita 5,000

July 23rd, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MALKIA wa mbio za mita 5,000 kwenye Riadha za Dunia na Jumuiya ya Madola, Hellen Obiri aliweka rekodi mpya ya kitaifa katika mbio za maili moja jijini London nchini Uingereza, Julai 22, 2018.

Obiri alikamilisha umbali huo wa kilomita 1.6 katika nafasi ya tatu kwa dakika 4:16.15 akifuta rekodi ya dakika 4:16.56 aliyoweka katika London Grand Prix nchini Uingereza mnamo Julai 9 mwaka 2017.

Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 28 alimaliza nyuma ya mshindi Mholanzi Sifan Hassan na nambari mbili Muethiopia Gudaf Tsegay waliotumia dakika 4:14.71 na 4:16.14, mtawalia.

Mkenya Emmanuel Korir alitawazwa mshindi wa mbio za mita 800. Korir, 23, alishinda duru hii ya 11 kwa dakika 1:42.05, ambayo ni kasi ya juu katika mbio hizi za mizunguko miwili tangu mwaka 2012.

Baadhi ya wakimbiaji waliobwagwa na Korir ni Mbotswana Nijel Amos, ambaye alikuwa ametimka kasi ya juu mwaka huu ya dakika 1:42.14 mjini Monaco mnamo Julai 20.

Bingwa wa Jumuia ya Madola Wycliffe Kinyamal alijaribu kupokonya Mkenya mwenzake Korir taji katika mita 200, lakini bila mafanikio. Korir, ambaye pia alivunja rekodi ya Riadha za Diamond League ya duru ya London, ameingia katika orodha ya wakimbiaji sita-bora walio na kasi ya juu katika mbio za mita 800 duniani.

Kinyamal alipitwa na Muamerika Clayton Murphy kwenye laini, lakini wote wakapata muda mmoja wa dakika 1:43.12. Amos alikamilisha katika nafasi ya nne kwa dakika 1:43.29.

Mkenya Justus Soget alimaliza mbio za mita 1,500 nyuma ya bingwa Matthew Centrowitz kutoka Marekani na nambari mbili raia wa Australia Ryan Gregson.

Nao Lilian Kasait na Cyrus Rutto walikuwa Wakenya wa kwanza kumaliza mbio za mita 3,000 na mita 5,000 Julai 21 baada ya kushikilia nafasi ya kwanza na sita, mtawalia.