Michezo

Obiri, Cheruiyot waendea mataji ya Diamond League wakikabiliwa na ushindani mkali

September 5th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

WAKIMBIAJI nyota Hellen Obiri (mita 5,000) na Timothy Cheruiyot (mita 1,500) watapata ushindani mkali katika kampeni zao za kutetea mataji ya Riadha za Diamond League jijini Brussels nchini Ubelgiji, Ijumaa.

Bingwa wa dunia Obiri, 29, ambaye alitwaa mataji ya Diamond League mwaka 2017 na 2018, atapimwa vilivyo uweledi wake katika mbio hizo za mizunguko 12 na nusu na Mholanzi Sifan Hassan, ambaye ni mshindi wa Bara Ulaya na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya maili moja.

Obiri, ambaye anaongoza jedwali kwa alama 19, nne pekee mbele ya Hassan, pia atashindania taji la Brussels dhidi ya Mkenya mwenzake Beatrice Chepkoech, ambaye ni mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji na alihifadhi taji lake mjini Zurich nchini Uswizi mnamo Agosti 29.

Agnes Tirop, ambaye alibwaga Obiri katika mbio za mita 5,000 katika duru ya Stockholm nchini Uswidi pamoja na katika mbio za mita 10,000 katika mashindano ya kitaifa ya Kenya wiki chache zilizopita, pia ni mmoja wa wakimbiaji wanaopigiwa upatu kuwania taji.

Tirop anashikilia nafasi ya pili nyuma ya Obiri kwa alama 17. Nafasi nane za kwanza kwenye kila duru hutunukiwa alama nane, saba, sita, tano, nne, tatu, mbili na moja, mtawalia. Inamaanisha kuwa vita vya kuwania taji la msimu huu katika kitengo hiki bado viko wazi kwa angaa wakiambiaji wanne – Obiri, Tirop, Hassan na Caroline Kipkirui, ambaye amezoa alama 13.

Mjerumani Konstanze Klosterhalfen na Waethiopia Fantu Worku na Letesenbet Gidey, ambao wana alama saba, saba na sita mtawalia, pia watatifua vumbi katika kitengo hiki.

Obiri alianza mwaka 2019 vyema kwa kushinda Mbio za Nyika za Dunia (Denmark), mbio za kilomita 10 za Great Manchester (Uingereza) na duru ya Doha nchini Qatar, lakini ametapatapa. Anajivunia muda bora katika mbio za mita 5,000 mwaka huu wa dakika 14:20.36 kutoka ushindi wake wa taji la London nchini Uingereza mwezi Julai. Hata hivyo, Obiri atalazimika kufanya kazi ya ziada mjini Brussels anapojiandaa pia kupeperusha bendera ya Kenya katika Riadha za Dunia nchini Qatar mwisho wa mwezi huu wa Septemba.

Cheruiyot alishinda mataji ya Diamond League ya mbio za mita 1,500 mwaka 2017 na 2018. Amekuwa katika hali nzuri msimu huu. Ameshinda mbio zote ameshiriki mwaka huu ikiwemo kutwaa taji la duru ya Lausanne nchini Uswizi kwa kasi ya juu mwaka huu ya dakika 3:28.77. Cheruiyot anashikilia nafasi ya pili kwenye jedwali la mwaka huu kwa alama 31, mbili nyuma ya Djibouti Ayanleh Souleiman anayeongoza kwa alama 33.

Cheruiyot atakutana na Souleiman pamoja na nambari tatu Jakob Ingebritsen kutoka Norway, ambaye amezoa alama 26, Mganda Ronald Musagala (alama 12), ambaye alinyakua mataji ya Paris na Birmingham wakati Mkenya huyo hakuwa.

Kivumbi pia kinatarajiwa katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji za wanaume ambazo zimevutia bingwa wa Diamond League mwaka 2016, 2017 na 2018 Conseslus Kipruto.

Mkenya huyu hajakuwa katika hali nzuri msimu huu tangu aibuke mshindi miezi 12 iliyopita akivalia kiatu kimoja baada ya kiatu kingine kutoka.

Bingwa huyu wa Afrika, Jumuiya ya Madola, Dunia na Olimpiki alishiriki mbio zake za kwanza za Diamond League msimu huu jijini Paris nchini Ufaransa akimaliza katika nafasi ya tano kwa dakika 8:13.75 mnamo Agosti 24. Alijiondoa kutoka michezo ya Afrika (African Games) nchini Morocco siku mbili baadaye. Anashikilia nafasi ya 11 kwa alama nne pekee kwa hivyo taji la mwaka 2019 linaonekana litapata mshindi mpya.

Soufiane El Bakkali (Morocco), Benjamin Kigen (Kenya) na Chala Beyo (Ethiopia) wanashikilia nafasi tatu za kwanza kwa alama 24, 21 na 17, mtawalia. Bakkali alibeba mataji ya Doha, Monaco na Paris, lakini alizidiwa maarifa na Kigen mjini Rabat katika michezo ya Afrika. Kigen pia ameandikisha matokeo mseto msimu huu.