Habari Mseto

Obure na Ouko kujua hatima yao Jumatatu ijayo

September 14th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu itaamua Jumatatu ijayo ikiwa itawaachilia kwa dhamana washtakiwa wawili waliokana kumuua muuzaji magari Kelvin Omwenga mnamo Agosti 21,2020 katika mtaa wa Kilimani Nairobi.

Jaji Jessie Lesiit aliombwa na mawakili Prof P L O Lumumba na Kennedy Arum awaachilie kwa dhamana Chris Philip Obure anayeshtakiwa pamoja na mlinzi wake Robert John Ouko Bodo.

Prof Lumumba alimweleza Jaji Lesiit kuwa wawili hao tayari wamepewa dhamana ya Sh50,000 pesa tasilimu na hakimu mkazi Sinkiyian Tobiko katika kesi ya matumizi mabaya ya silaha.

Jaji Lesiit pia alielezwa Jaji James Wakiaga alikuwa amewaachilia kwa dhamana ya Sh500,000 kabla ya kufunguliwa mashtaka ya mauaji ya Omwenga.

Prof Lumumba alisema washtakiwa hawa hawatatoroka na kwamba watafika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi.

Mahakama ilifahamishwa washtakiwa walijisalamisha kwa Polisi baada ya kisa hicho cha mauaji katika mtaa wa Galana Kilimani Nairobi.

Lakini ombi hilo lilipingwa na afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Bi Gikui Gichuhi.

Bi Gichuhi alisema washtakiwa watavuruga mashahidi endapo wataachiliwa kwa dhamana. Jaji Lesiit atatoa uamuzi mnamo Septemba 21,2020.

Wiki iliyopita Jaji Mumbi Ngugi alitupilia mbali ombi la Obure la kugeuzwa shahidi mkuu wa Serikali akidai Ouko aliiba bastola yake akaenda kutekeleza uhalifu nayo.

Mawakili Prof P L O Lumumba (kushoto mwenye suit nyeusi) na Kennedy Arum (kati) wanaowakilisha Ouko na Obure. Picha/RICHARD MUNGUTI

“Ombi hili la Obure halina mashiko kisheria. Inalenga kuyumbisha uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ashtakiwe kwa mauaji ya Kevin Omwenga mnamo Agosti 21 katika makazi yake Galana Suits eneo la Kilimani Nairobi,” alisema Jaji Ngugi.

Jaji huyo alisema mahakama kamwe haiwezi kuvuruga utenda kazi wa DPP.

Alisema wawili hao wameshtakiwa kwa mauaji na kamwe korti haiwezi kuingilia uhuru wa DPP chini ya kifungu nambari 157 cha katiba cha kuwashtaki washukiwa.

Mahakama ilisema katiba imempa DPP idhini ya kufungulia mshukiwa kesi kulingana na ushahidi alio nao.

“Katika kesi hii mwanaume alipoteza maisha na lazim kesi iendelee,” alisema Jaji Ngugi.

Jaji huyo alisema Obure atakuwa na fursa mbele ya Jaji atakayesikiza kesi hiyo kuwasilisha ushahidi anaodai DPP angeliuzingatia kwanza kabla ya kumshtaki pamoja na Ouko.

Katika ombi lake kupitia kwa wakili Danstan Omari ,Obure alidai bastola yake iliyotumika kumuua Omwenga iliibwa na mlinzi wake , Ouko wanayeshtakiwa pamoja.

Wawili hao walikana walishirikiana kumuua Omwenga. Jaji Ngugi aliwaruhusu mawakili Prof P L O Lumumba na Otieno Arum kuwasilisha ombi la wawili hao kuachiliwa kwa dhamana.

“Wawili hawa wameruhusiwa kuwasilisha ombi la kuachiliwa kwa dhamana mnamo Jumatatu (Septemba 14, 2020),”alisema Jaji Ngugi.

DPP kupitia kwa Bi Gikui Gichuhi aliomba korti itupilie mbali ombi la Obure.