Obure na Ouko taabani kwa mashtaka ya kumuua Kelvin Omwenga

Obure na Ouko taabani kwa mashtaka ya kumuua Kelvin Omwenga

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA Chris Philip Obure pamoja na mlinzi wake Robert John Ouko Bodo wanaozuiliwa kwa mauaji ya Kelvin Omwenga watajua hatma yao Jumanne.

Hakimu mwandamizi wa mahakama ya Kibera Bw Derrick Kuto aliamuru Mabw Obure na Ouko wasalie katika kituo cha Polisi cha Kilimani hadi leo atakapoamua ikiwa ataruhusu polisi wawazuilie kwa siku 14.

Ombi la kuzuiliwa kwa wawili hao liliwasilishwa na afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ODPP) kupitia kwa Bw Allan Mogere.

Bw Mogere aliomba wawili hao wazuiliwe kwa siku 14 kuwezesha polisi kukamilisha uchunguzi wa kesi ya mauaji watakayoshtakiwa.

Mahakama ilielezwa wawili hao watapelekwa kupimwa akili ibainike utimamu wao kabla ya kushtakiwa kwa mauaji ya Omwenga, aliyekuwa na umri wa miaka 28.

Pia mahakama ilielezwa polisi wanataka kuwahoji na kuandikisha taarifa ya watu wanne waliokuwa na marehemu usiku wa Agosti 22, 2020 katika makazi yake yaliyo katika jengo la Galana lililoko Kilimani, Nairobi.

Hakimu mwandamizi Derrick Kuto. Picha/RICHARD MUNGUTI

Bw Kuto alielezwa kuwa polisi wanataka kukagua bastola iliyotumika na pia kukagua picha za CCTV zinazoonyesha Bw Ouko akiingia na kutoka katika makazi ya Omwenga.

Pia uchunguzi wa maiti ya Omwenga haujafanywa.

Lakini mawakili Profesa P L O Lumumba na Otieno Arum walipinga ombi la kuzuiliwa kwa washukiwa hao siku 14 wakisema , “ uchunguzi unaofanywa haupasi kuchukua siku hizo 14.”

Walisema washtakiwa walijisalamisha kwa polisi na wako tayari kushirikiana na polisi kukamilisha uchunguzi.

“Washtakiwa hawatavuruga uchunguzi wa kesi hii na wako tayari kuwasiliana na polisi wanaochunguza kesi hii,” alisema Prof Lumumba.

Prof Lumumba alisema bastola iliyotumika katika mauaji ya Omwenga ni yake aliyopewa na idara husika ya kikosi cha polisi.

“Kwa vile mahakama ilianza kusikiza kesi saa saba sina muda wa kutosha kutayarisha uamuzi. Nitautoa kesho (leo) saa nane mchana,” alisema Bw Kuto.

You can share this post!

Vijana 56,000 kufaidika na mkopo wa Sh800,000 kila vijana...

BI TAIFA AGOSTI 1, 2020