Michezo

Ochan, Sichenje watia saini kandarasi mpya Ingwe huku sajili wapya wa Gor wakipata vibali vya FIFA

October 19th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO mkabaji Collins Sichenje na kipa Benjamin Ochan wamerefusha vipindi vya kuhudumu kwao kambini mwa mabingwa mara 13 wa Ligi Kuu ya Kenya, AFC Leopards.

Sawa na Sichenje, Ochan ambaye ni raia wa Uganda, ametia saini mkataba mpya utakaomshuhudia akiendelea kuwa tegemeo langoni pa Leopards kwa mwaka mmoja zaidi.

Sichenje, 19, aliingia katika sajili rasmi ya Leopards mnamo Septemba 2019 baada ya kuagana na kikosi cha Green Commandos cha Shule ya Upili ya Kakamega; Kakamega High School.

“Kubwa zaidi katika maazimio yangu msimu huu ni kushirikiana vilivyo na wanasoka wenzangu na kunyanyulia Leopards ufalme wa Ligi Kuu ambao umekuwa ukiwahepa tangu 1998. Nalenga pia kuwa miongoni mwa wachezaji bora zaidi ligini,” akasema Sichenje.

Ochan alisajiliwa na Leopards kutoka Kabwe Warriors ya Zambia mnamo Julai 2019.

“Hatua ya Ochan kurefusha mkataba wake nasi ni afueni kubwa. Mbali na kuwa kipa bora zaidi ligini kwa sasa, ana sifa za uongozi, tajriba pevu na uzoefu mkubwa katika ulingo wa soka,” akasema kocha wa Leopards, Anthony Kimani.

Leopards wanatazamiwa kumpa mikoba kocha wa zamani wa Township Rollers nchini Botswana, Thomas Trucha, ili kujaza nafasi ya Kimani anayetarajiwa kuagana na Ingwe kwa minajili ya kujiendeleza zaidi kimasomo.

Kwa mujibu wa ratiba mpya ya Ligi Kuu ya msimu 2020-21 iliyotolewa na Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wiki jana, Leopards wamepangiwa kufungua muhula dhidi ya Western Stima mnamo Novemba 20 kabla ya kuvaana na Bidco United, Zoo, Nzoia Sugar na mshindi wa mchujo kati ya Kisumu Allstars na Vihiga United kwa usanjari huo.

Kati ya wachezaji wapya walioingia kambini mwa Leopards muhula huu na ambao watatambulishwa rasmi kwa mashabiki wiki hii, ni Harrison Mwendwa, Peter Thiong’o na Washington Munene waliobanduka kambini mwa Kariobangi Sharks, Kakamega Homeboyz na Nairobi Stima mtawalia. Sogora wa kigeni aliyeingia kambini mwa Leopards msimu huu ni Fabrice Mugheni kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).

Kufikia sasa, Leopards wamethibitisha kuagana rasmi na wavamizi Vincent Oburu na Christopher Oruchum walioyoyomea Wazito FC na Tusker FC mtawalia.

Baada ya kuchuana leo na Shabana FC kwenye gozi la kuwania ubingwa wa Mashujaa Day Cup ugani Gusii, Leopards wanatarajiwa kupiga kambi mjini Eldoret kisha Kakamega kwa minajili ya kujiandaa kwa kampeni za msimu ujao wa 2020-21. Mechi zao za kujifua zitadhaminiwa na kampuni ya Galana Oil Kenya.

Wakati uo huo, sajili wanne wapya wa Gor Mahia wameidhinishwa sasa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuchezea mabingwa hao watetezi na washindi mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya.

Jules Ulimwengu (Rayon Sports, Burundi), Tito Okello (Vipers, Uganda), Mcameroon Bertrand Konfor (Al Mudhabi, Oman) na John Macharia (FC Guria Lanchkhuti, Georgia) wamepokea vyeti vya uhamisho wa kimataifa (ITC) kutoka FIFA na vibali vya kufanyia kazi nchini Kenya.

Kuidhinishwa kwao kunawapa Gor Mahia uhuru wa kuwasajilisha kwa kampeni zijazo za kimataifa za Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika (CAF) kuanzia Oktoba 21.