Habari Mseto

OCS aitwa kortini kueleza raia wa Uganda alivyotoweka

May 19th, 2020 1 min read

Na Richard Munguti

AFISA mkuu wa kituo cha Polisi cha Kamukunji (OCS) Jumanne aliagizwa afike katika mahakama ya Milimani Jumatano kueleza jinsi raia wa Uganda anayeshtakiwa kwa kumteka nyara afisa wa polisi Konstebo Abel Misati miezi minne iliyopita, alivyotoweka.

Hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot alimwamuru OCS huyo afike kortini “kueleza jinsi Martin Wasike alivyotoweka.” Na wakati huo huo Bw Cheruiyot alitoa kibali cha kumtia nguvuni Wasike.

Wasike alishtakiwa Mei 11, 2020 pamoja na raia mwingine wa Uganda Sharrif Wanabwa pamoja na raia wa Kenya Phoebe Anindo Andayi.

Wakili Alfred Nyandieka. Picha/ Richard Munguti

Watatu hao Wasike, Wanabwa na Phoebe waliamriwa wazuiliwe katika kituo hicho cha Kamkunji hadi Juni 2, 2020 kuhojiwa kuhusu kutoweka kwa Konst Misati.

Misati alitoweka Januari 19, 2020 na kufikia sasa hajulikani aliko.

Bw Cheruiyot alielezwa na wakili Alfred Nyandieka anayewakilisha familia ya Abel kuwa “inahofiwa aliuawa kwa vile miezi minne imepita tangu atoweke.”

Bw Nyandieka alisema ni “OCS tu atakayeeleza alivyotoroka Wasike ikilitiliwa maanani seli za Polisi zimejengwa kwa njia nzuri na kila wakati zinalindwa na afisa aliyejihami na bunduki.”

Mahakama ilijulishwa na afisa anayechunguza kesi hiyo kwamba “ripoti ya kutoweka kwa Wasike imepelekwa kwa vituo vyote ya mipakani pamoja na picha yake akionekana akamatwe.”

Kiongozi wa mashtaka aliomba OCS aagizwe afike kortini Jumatano.

Hakimu mwandamizi Kennedy Cheruiyot… Picha/RICHARD MUNGUTI

“Kufuatia kutoroka kwa Wasike naamuru OCS Kamkunji afike kortini Jumatano kueleza jinsi alivyotoweka,” Bw Cheruiyot aliagiza.

Wasike, Wanabwa na Andayi wameshtakiwa kumteka nyara Abel Misati Januari 19 2020 kwa lengo la kumuua.

Pia walikana kupatikana wakitumia simu yake ya rununu katika mtaa wa Eastleigh Nairobi.

Mahakama ilikataa kuwaachilia watatu hao kwa dhamana ikisema “watatoroka na hawana vitambulisho.”