Habari Mseto

OCS anayedaiwa kuua mwanafunzi kuzidi kuzuiliwa kituoni

May 15th, 2018 1 min read

Na VICTOR RABALLA

AFISA wa polisi wa cheo cha juu aliyedaiwa kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu katika mtaa wa Mamboleo mjini Kisumu, atasalia kizuizini kwa siku saba ili kutoa nafasi ya uchunguzi zaidi na kumzuia kuvuruga ushahidi.

Hakimu Mkazi wa Winam, Bi Caroline Njalale, aliagiza mkuu huyo wa polisi wa kituo cha Kehancha, Bw Sebastian Ambani, azuiliwe katika kituo cha polisi cha Maseno kama ilivyoombwa na afisa wa upelelezi, Bw Alfred Shibeka.

Kulingana na Bw Shibeka, OCS huyo alikuwa ametuma jamaa zake kwenda kutisha familia ya marehemu Brian Chacha.

Hakimu alisema siku saba zinatosha kukamilisha upelelezi kabla kesi hiyo kutajwa Mei 21.

“Nimesikia ombi na majibu kutoka kwa mshtakiwa na kwa manufaa ya pande zote mbili, ninaagiza azuiliwe katika kituo cha polisi cha Maseno,” akasema Bi Njalale.

Bw Shibeka alisema kuwa kuzuiliwa kwa Bw Ambani ni kwa manufaa ya familia ya marehemu ambayo imekuwa ikitatizika tangu kuuawa kwa mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 22, Alhamisi iliyopita.

“Hata kukamatwa kwake kulitokana na malalamishi ya wananchi ambao waliandamana hadi katika kituo cha polisi cha Mamboleo Ijumaa iliyopita,” akasema.

Ambani alikanusha madai ya kuwatisha mashahidi alisema anateseka kizuizini.