Michezo

Odera akanusha anataka kutoroka Simbas kujiunga na Shujaa

June 25th, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji 15 kila upande Paul Odera amepuuzilia mbali madai kuwa anamezea mate wadhifa wa kocha mkuu wa timu ya Kenya ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa.

Katika mahojiano Alhamisi, kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 ameambia Taifa Leo: “Kuna uvumi mwingi tu unaenezwa. Mimi sikutuma ombi la kuwa kocha mkuu wa timu ya Shujaa.”

Odera, ambaye ni mwalimu wa shule ya Peponi House Preparatory jijini Nairobi, amesema kuwa lengo lake ni kuongoza Simbas katika kampeni za kufika Kombe la Dunia 2023.

“Lengo langu ni Kombe la Dunia 2023 la raga ya wachezaji 15 kila upande nchini Ufaransa,” anasema kocha huyo aliyeongoza timu ya chipukizi ya Kenya almaarufu Chipu mwaka 2019 kupiga miamba Namibia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2005 na kuingia Kombe la Dunia la daraja ya pili la makinda (JWRT) lililofanyika nchini Brazil.

Alipoulizwa kuthibitisha habari zinazosambaa kuwa Odera yuko mstari wa mbele kutwikwa majukumu ya Shujaa, Mwenyekiti wa Shirikisho la Raga Kenya (KRU) Oduor Gangla amesema “sina habari kuhusu hilo.”

Wadhifa wa kocha mkuu wa Shujaa uliachwa wazi baada ya raia wa New Zealand Paul Feeney kuondoka Juni 12.

Feeney alisaidiwa na kocha wa klabu ya Mwamba, Kevin ‘Bling’ Wambua ambaye huenda akatwikwa majukumu hayo baada ya Wakenya Benjamin Ayimba, Felix Ochieng’, Innocent Simiyu, Mitch Ocholla na Paul Murunga kuwa kileleni miaka ya hivi karibuni.

KRU inatafuta kocha Mkenya kuongoza Shujaa kwa mashindao ya kifahari ya Raga ya Dunia pamoja na mashindano mengine ya kimataifa.

Kazi hii inahitaji kocha kujukumika wakati wote. Inamaanisha kuwa Odera atalazimika kuacha ualimu kwa muda atakaoongoza Shujaa.

Odera alicheza raga kati ya mwaka 1986 na 2005 alipostaafu uchezaji baada ya kupata jeraha mbaya la shingo. Mchezaji huyo wa zamani wa klabu za Barclays Bank na Kenya Harlequin alianza kazi ya ukocha mwaka 1994 akiwa mchezaji kabla ya kuzamia shughuli hiyo kabisa alipostaafu kucheza.