Michezo

Odera ataja wachezaji watano wapya kwa mechi ya Victoria Cup dhidi ya Zambia

August 23rd, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Paul Odera ametaja wachezaji watano wapya katika timu ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Simbas itakayoalika Zambia jijini Nairobi mnamo Agosti 24 kwa mechi ya raga ya Victoria Cup.

Francis Mwita, Brian Amaitsa, Samuel Asati na Eliud Mulakoli wataanza mechi dhidi ya Zambia naye Ian Njenga yumo mbioni kushiriki mchuano huo kutoka kitini.

Odera bado hajaonja ushindi kama kocha mkuu wa timu hii ya watu wazima baada ya kukosa ushindi wa Simbas wa alama 16-5 dhidi ya Uganda mnamo Julai 13 na dhidi ya Zambia 43-23 mjini Kitwe mnamo Julai 27.

Katika ushindi hizo mbili, Simbas ilikuwa chini ya kocha msaidizi Albertus Van Buuren. Odera alikosa mechi ya Kampala akiwa na majukumu ya timu ya taifa ya chipukizi almaarufu Chipu nchini Brazil na pia mechi dhidi ya Zambia akiwa tu ndiyo amerejea kutoka ziara hiyo ya Amerika Kusini akiwa na uchovu.

Hata hivyo, alihusika pakubwa katika kuchagua kikosi kilichoshiriki mechi hizo. Mechi yake ya kwanza kama kocha mpya wa Kenya Simbas iliishia kuwa kichapo cha alama 16-13 uwanjani Mamboleo mjini Kisumu mnamo Juni 22. Alijiunga na Simbas nchini Zimbabwe kwa mechi nyingine ya Victoria Cup mnamo Agosti 4. Kenya ililemewa 30-29 na Zimbabwe mjini Bulawayo.

Okwach, Silungi na Okoth wanarejea kikosini baada ya kuchezea Simbas mnamo Juni 22 katika mechi hiyo ya mkondo wa kwanza ya Elgon Cup.

Curtis Lilako ameteuliwa kuwa nahodha na atasaidiwa na Elkeans Musonye na Jacob Ojee wote ambao wataanza mechi.

“Hatubadilishi mbinu zetu za kushambulia na ulinzi kwa sababu tukifanya hivyo tutakanganya wachezaji. Tunajitahidi kuwafanya wawe bora tunapoendelea na mashindano haya. Talanta si tatizo katika nchi hii, kile tunachofaa kuwazia ni falsafa katika timu zetu za taifa,” alisema Odera akizindua kikosi cha Kenya jijini Nairobi, Alhamisi.

“Naamini tuko tayari kwa mechi ya Jumamosi. Kuna mshikamano mzuri kati ya wachezaji chipukizi na wale wazoefu. Kiu ya timu hii inaweza tu kuonekana uwanjani kwa hivyo tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa msukumo zaidi,” Lilako alisema.

Hii ni mara ya kwanza Kenya inaandaa mechi ya raga ya Victoria Cup inayorejea baada ya miaka saba. Katika mechi ya mwisho iliyochezewa jijini Nairobi, Kenya ilicharazwa 26-21 na Zimbabwe mnamo Julai 23 mwaka 2011 uwanjani Nyayo.

Bei ya tiketi za kawaida ni Sh500, huku zile za VIP zikiuuzwa Sh1000.

Kikosi cha Simbas

Wachezaji 15 wa kwanza: Oscar Simiyu, Toby Francombe, Curtis Lilako (nahodha), Francis Mwita*, Malcolm Onsando, Brian Amaitsa*, Monate Akuei, Elkeans Musonye (nahodha msaidizi), Samuel Asati*, Charles Kuka, Geoffrey Okwach, Johnstone Mung’au, Eliud Mulakoli*, Jacob Ojee (nahodha msaidizi), Isaac Njoroge.

Wachezaji wa akiba: Griffin Musila, Ian Njenga*, Melvin Thairu, Simon Muniafu, Emmanuel Silungi, Samson Onsomu, Anthony Odhiambo, John Okoth.