Michezo

Odera kuongoza wanaraga wa Kenya Simbas kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Ufaransa

November 6th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KENYA ni miongoni mwa mataifa yanayojivunia vikosi thabiti na imara zaidi katika ulingo wa raga ya wachezaji saba kila upande duniani na timu ya taifa ya Kenya ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, imekuwa ikishiriki kampeni za Raga ya Dunia za HSBC World Sevens kwa muda mrefu na kuwa tishio kwa wapinzani wao wakuu.

Kenya ambayo inafahamika zaidi duniani kwa sababu ya umahiri wa wanariadha wake, imeanza pia kutanua kifua kwenye vipute cha raga ya kimataifa kwa wachezaji saba kila upande na ilitinga fainali za Kombe la Dunia za 2009 na 2013 zilizoandaliwa Dubai na Moscow mtawalia.

Baada ya kufuzu kwa michezo ya Olimpiki ya Rio 2016 nchini Brazil, Shujaa kwa sasa wanajiandaa kunogesha Olimpiki za Tokyo, Japan mnamo Julai 2021.

Licha ya ufanisi huo wa Shujaa, Kenya haijatamba vilivyo kwenye ulingo wa raga ya wachezaji 15 kila upande huku timu ya taifa katika mchezo huo, Simbas, ikipania kufuzu kwa fainali za Raga ya Dunia (RWC) ambazo huandaliwa kila baada ya miaka minne kwa mara ya kwanza katika historia.

Afrika Kusini ambao ni wapinzani wakuu wa Kenya barani Afrika walitawazwa mabingwa wa Kombe la Dunia kwa wanaraga 15 kila upande mwaka wa 2019 nchini Japan.

Kwa mujibu wa kocha Paul Odera wa Kenya Simbas, kikosi chake kina kiu ya kufuzu kwa kivumbi cha RWC ambacho kitaandaliwa nchini Ufaransa mwaka ujao wa 2021.

Baada ya mabingwa watetezi Afrika Kusini kushindwa kufuzu kwa fainali zijazo za RWC, matumaini ya Kenya na vikosi vingine vinavyowania fursa ya kunogesha kivumbi hicho ni kutwaa kwanza ubingwa wa bara la Afrika.

Namibia waliwahi kunyima Kenya Simbas fursa ya kufuzu kwa fainali za RWC mara mbili katika makala ya 2015 na 2019.

Odera ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Chipu, alipokezwa mikoba ya Kenya Simbas mnamo Disemba 2019.

“Tutapania sasa kutumia teknolojia kuteua wanaraga bora zaidi watakaounga kikosi cha Simbas. Hata mchezaji akiwa Australia, Afrika Kusini au Uingereza, tutakuwa na kanzi yao na itakuwa rahisi kuwafuatilia na kutathmini maendeleo yao kabla ya kupata kikosi cha kuwajibisha katika mashindano ya haiba kuu,” akasema Odera.

Odera alipokezwa mikoba ya Simbas baada ya kuongoza Chipu kupiga Namibia na kunyanya ubingwa wa Barthes Cup mnamo 2019.

Wasaidizi wa Odera katika benchi ya kiufundi ya Kenya Simbas kwa sasa ni pamoja na Jimmy Mnene (Meneja wa timu), Ben Mahinda (kocha wa mazoezi), Edwin Boit (mchanganuzi wa kikosi), Michael Owino (kocha wa viungo vya mwili) na Albertus Van Buuren (kocha msaidizi).

Odera ambaye ana cheti cha Raga ya Dunia ya kiwango cha Level 3 katika ukufunzi pia ni mwalimu katika Shule ya Peponi jijini Nairobi.