Michezo

Odhiambo atia saini kandarasi ya miaka miwili KCB

August 19th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

KIUNGO wa Harambee Stars, Dennis Odhiambo amejiunga na KCB inayoshiriki Ligi Kuu ya KPL kwa mara ya pili baada ya kurejea mapema msimu uliopita.

Kiungo huyo aliyevunja ndoa yake na Sofapaka FC mwezi uliyopita amekuwa akiwindwa na timu kadhaa ikiwamo Gor Mahia FC na Wazito FC.

Odhiambo ametia wino kandarasi ya miaka miwili ambapo amejiunga na Stephen Waruru pia Pascal Ogweno kati ya wachezaji waliotemwa na Gor Mahia FC mwishoni mwa msimu uliyopita na kumfuata kocha mpya wa KCB, Zedekiah Otieno aliyekuwa naibu wa kocha wa Gor Mahia FC. Waruru na Ogweno nao pia walisajiliwa na KCB kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Kocha mpya anayesadiana na kocha, Godfrey Oduor alipokezwa mikoba kuiongoza KCB baada ya kocha Frank Ouna kuondoka.

”Tunaendelea kuunda kikosi imara tayari kutifua kivumbi kikali kwenye kampeni za muhula ujao huku tukikusudia kumaliza miongoni mwa nafasi bora kwenye jedwali,” ofisa mkuu wa KCB, Paul Russo alinukuliwa akisema.

Itakumbukwa kuwa kocha wa Harambee Stars aliyeondoka, Sebastien Migne alimtwika Dennis Odhiambo jukumu la unahodha wa kikosi hicho kwenye mechi za kufuzu kushiriki pambano la Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) walipobandualiwa katika hatua ya kwanza na Tanzania baada ya kushindwa kupitia mipigo ya penalti Uwanjani Kasarani hapa nchini.

Kando na Sofapaka FC kiungo huyo pia amefanikiwa kusakatia timu tofauti hapa nchini ikiwamo Thika United. Kwenye jedwali ya KPL msimu uliyopita, KCB ilimaliza ya kumi kwa alama 45, mbili mbele ya AFC Leopards.